Na
Baraka Mpenja , Dar es
salaam
0712461976
au 0764302956
MABINGWA
watetezi wa ligi kuu soka Tanzana bara, Young Africans leo jioni wanatarajia
kufanya mazoezi katika uwanja wa Ally Hassan Mwinyi , mjini Tabora kujiwinda na
mchezo wa kesho dhidi ya wenyeji, Rhino Rangers.
Yanga
waliwasili mjini Tabora jana usiku wakiwa na tafakuri nzito ya kutafuta pointi
tatu muhimu ili kuwasogelea Azam fc waliopo kileleni katika msimamo wa ligi.
Mpaka
sasa Yangaa wapo nafasi ya pili wakiwa na pointi 40 baada ya kucheza mechi 19,
wakati Azam fc wameshajikusanyia pointi 44 kileleni kwa kushuka dimbani mara 20.
Timu
hizi mbili zilitoka sare ya bao 1-1 jumatano ya wiki hii katika mchezo
uliochezwa uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Hata
hivyo, Azam fc walionekana kuwa bora zaidi kwani kwa dakika 20 za mwisho
walicheza wakiwa pungufu kufuatia beki wake wa kulia, Erasto Edward Nyoni
kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwasababu ya kutoa lugha chafu kwa mwamuzi.
Azam
fc hawajafungwa mechi hata moja msimu huu, na malengo yao ni kutwaa ubingwa.
Kocha
wa Yanga, Mholanzi, Hans Van Der Pluijm baada ya mechi ya jumatano alisema anajipanga kufanya vizuri mechi ya
kesho na nyingine zote zilizosalia.
Kushinda
kwa Yanga hapo kesho kutawafanya warudishe hadhi yao ya kutetea ubingwa msimu
huu,
Wakati
Yanga wakihitaji ushindi ili kujiweka mazingira mazuri ya kutwaa taji, wenyeji
wao, Rhino wanahangaika kukwepa mkasi wa kushuka daraja.
Kikosi
hicho cha kocha Jumanne Chale mpaka sasa kinaburuza mkia kwa kujikusanyia
pointi 13 kufuatia kushuka dimbani mara 21.
Rhino
wamebakiza mechi 5 ambazo wanahitaji kushinda zote ili kurejesha matumaini,
japokuwa inaonekana kuwa ndoto.
Kwa
hesabu za haraka, maafande hawa wa JWTZ kama vile wameshashuka daraja, ingawa
mpira wa miguu huwa hauendi kwa hesabu rahisi kiasi hiki.
Kama
Rhino watashinda kesho na mechi nyingine zote zilizobaki, basi wanaweza
kufikisha point 28 ambazo pengine zitaweza kuwaokoa.
Kushinda
mechi zote itakuwa ngumu hasa kwa kuanzia na kipute cha kesho dhidi ya Yanga wenye uhitaji mkubwa wa
Pointi kwasasa.

Mechi
nyingine yenye msisimko hapo kesho ni baina ya JKT Ruvu dhidi ya Mbeya City
katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Mechi
hii ni muhimu kwa timu zote kwani JKT Ruvu wapo katika harakati za kukwepa
kushuka daraja.
Kwasasa
kocha wake, Fredy Felix Minziro hana cha kupoteza zaidi ya kutafuta ushindi.
Hivyo wataingia uwanjani kwa nguvu zote.
Haitakuwa
kazi nyepesi kwa Minziro kupata matokeo mazuri hapo kesho, kwasababu Mbeya City
wanahitaji zaidi pointi ili kujikita katika nafasi za juu.
Mpaka
sasa Mbeya City wapo nafasi ya tatu kwa pointi 39, hivyo wakishinda kesho watafikisha
pointi 42.
Kupanda
nafasi itategemeana na matokeo ya Tabora ambapo Yanga watakuwa na kibarua na
Rhino.
Kama
Yanga atashindwa kupata matokeo ya ushindi na Mbeya City atashinda, basi
wanajangwani watazidi kujiweka mazingira hatari zaidi kwasababu wataporomoka
kwa nafasi moja.
Ligi
kuu itaendelea tena siku ya jumapili, ambapo uwanja wa Taifa, Simba SC watakuwa
wenyeji wa Coastal Union .
Hiyo
itakuwa mechi ngumu kwa timu zote kwasababu kocha wa Simba, Dravko Logarusic hahitaji
kuona anapata matokeo mabaya kwa mara nyingine.
Loga
ataingia akiwa na presha kubwa nyuma yake kutokana na ukweli kuwa Simba haijawa
katika ubora wake wa siku za nyuma.
Mpaka
sasa Mnyama yupo nafasi ya nne kwa pointi 36 kibindoni na ameshuka dimbani mara
21.
Nao
Coastal Union hawataki kufungwa tena ukizingatia wikiendi iliyopita walifungwa
mabao 4-0 na Azam fc uwanja wa Azam complex Chamazi.
Nao
vinara wa ligi hiyo, Azam fc watakuwa nyumbani kwao Azam complex kuumana na JKT
Oljoro.
Mechi
hiyo ni muhimu kwa Oljoro kwani wapo hatarini kushuka daraja msimu huu, hivyo
hawana cha kutafuta zaidi ya pointi tatu kwao.
Lakini
utakuwa muhimu zaidi kwa Azam fc, kwani kushinda kwao kutawafanya kuwa katika
mazingira mazuri ya kubeba ndoo ya ubingwa kwa mara ya kwanza.
Azam
fc wakishinda watazidi kusogelea ubingwa, lakini wakishindwa kupata matokeo
mazuri, Yanga wakashinda Tabora, basi watakuwa wamejitia hatiani.
Ruvu
Shooting watakuwa wenyeji wa Ashanti United Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani
Pwani.
0 comments:
Post a Comment