


Na Lulu Mussa na Rashda Swedi,
Ofisi ya Makamu wa Rais, Dar es Salaam
Serikali inaendelea na jitihada za kutoa elimu kwa umma juu ya njia bora za kuhudumia majokofu na viyoyozi ili kulinda tabaka la Ozoni.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Eng. Angelina Madete wakati wa ufunguzi wa Warsha ya Mafunzo kwa Wakufunzi kutoka Vyuo mbalimbali vya Ufundi Nchi.
Katika Hotuba yake Bi Madete amesema kuwa kemikali haribifu zinauwezo mkubwa kuharibu tabaka la Ozoni na kuongeza joto angani. Kutokana na sababu hizo, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na jamii za kimataifa zimekubaliana kufanya jitihada za kuondoa kemikali hizo hatarishi.
Bi Madete ameainisha baadhi ya kemikali hizo kuwa ni methyl bromide, halons na chloroflorocarbornsambazo hutumika kama vipozi katika majokofu, viyoyozi, vifaa vya kuzima moto, usafishaji chuma, ufukizaji wa mazao katika maghala na utengenezaji wa magodoro ambazo huleta madhara kwa tabaka la ozoni na adhari zake hutokea kwa binadamu, mimea na viumbe hai.
Katika awamu ya kwanza, Tanzania imefanikiwa kuondoka tani 296 za kemikali hizo haribifu ikiwa ni utekelezaji wa Mkataba wa Montreal na Vienna ambayo Tanzania iliridhia mwaka 1993.
Aidha, Bi Madete ameyataja madhara yatokanayo na uharibifu wa Tabaka la Ozoni kuwa ni kuongezeka kwa magonjwa ya saratani ya ngozi,uharibifu wa macho maarufu mtoto wa jicho, na upungufu wa uwezo wa mwili kujikinga na maradhi. Athari hizi kwa kiasi kikubwa zinatokana na shughuli za kibinadamu kama vile matumizi ya kemikali haribifu na zisizo rafiki kwa mazingira.
Warsha hii ya siku mbili imeratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais na inajumuisha wakufunzi kutoka Vyuo vya Ufundi vya Zanzibar na Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Kigoma, Mbeya na Mwanza.
0 comments:
Post a Comment