Dodoma. Mtafaruku ulioibuka juzi bungeni na kusababisha kusitishwa kwa kikao bila ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba, ulihitimishwa kwa maridhiano baada ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta kukutana na viongozi wa Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa) juzi usiku.
Baada ya maridhiano hayo, Sitta aliliambia Bunge jana kwamba alilazimika kufuta baadhi ya semina za masuala ya uelewa kuhusu Muungano ambazo zilipaswa kufanyika na kubakiwa na moja tu ya kupata uzoefu wa Kenya ambayo itatolewa kesho na magwiji wa Katiba wa nchi hiyo, akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya nchi hiyo, Amos Wako.
Juzi, baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo walimzuia Jaji Warioba kwa makelele na kugonga meza, wakidai kuwa Sitta alikuwa amekiuka kanuni kwa kumwalika Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba kabla ya Rais Jakaya Kikwete kulifungua Bunge.
Pia walidai kuwa kulikuwa na semina zilizokuwa zimeandaliwa kinyume na kanuni, ambazo zingewezesha kuingizwa misimamo ya baadhi ya vyama na kwamba Jaji Warioba alikuwa amepangiwa muda mfupi kinyume na ukubwa wa kazi aliyokuwa nayo. Awali, ilipangwa kuwa wajumbe wapate semina ya kujifunza zaidi kutoka kwa wakongwe juu ya masuala ya Muungano na historia ya nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar.
Waliotarajiwa kutoa semina hiyo ni Ramadhan Mapuri na Wadil Kavishe kutoka Zanzibar wakati kwa upande wa Bara walialikwa Hassan Ngwilizi na Profesa Issa Shivji.
Semina hiyo ilihojiwa na baadhi ya wajumbe ambao walisema CCM kinatumia nafasi hiyo kuwazima midomo kutoa maoni yao kwa uhuru. Habari za ndani zinaeleza kuwa katika maridhiano hayo, suala la Rais kuhutubia baada ya Jaji Warioba kuwasilisha hoja, lilikubaliwa liendelee kwa kuwa lingeleta usumbufu iwapo wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambao tayari walikuwa Dodoma, wangelazimika kumsubiri Rais Kikwete, Ijumaa.
Katiba hii itatumiwa na vizazi na vizazi, kwa vyovyote vile lazima itengenezwe kwa misingi ya kujali utu wa kila mtu, kuheshimiana, kuridhiana na kukubaliana. Ubabe na kukiuka kanuni kwa mwanya wa ‘busara za mwenyekiti’ havikubaliki. Mwenyekiti atumie busara pale tu ambako kanuni hazielekezi chochote.”
Sitta alisema: “Tumekubaliana pia kumwongezea muda Jaji Warioba, ili awasilishe hotuba yake.”
CHANZO: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment