Nahodha wa Azam fc, John Raphael Bocco `Adebayor na nahodha wa Yanga, Nadir Haroub `Canavaro`wakiwekana sawa ili kujua nani anaanzia kushambulia wapi. Bocco hakufunga leo hivyo kushindwa kuendeleza rekodi yake ya kuzifunga timu kubwa
Hawafungiki: Kikosi cha Azam fc leo hii kilicheza vizuri zaidi baada ya kuwa pungufu kufuatia kadi nyekundu ya Erasto Nyoni kwa kutoa lugha chafu kwa mwamuzi.
Kikosi cha Yanga leo hii kimepoteza penati baada ya Hamis Kiiza kukosa, lakini walipata nafasi kadhaa za kufunga, ila hawakuweza kuzitumia
Kocha msaidizi wa Azam fc, Kalimangonga Ongala (wa kwanza kulia) alisema safari ya ubingwa bado ni ndefu kwao. Wapili kutoka kulia ni kocha mkuu, Mcameroon, Joseph Marius Omog akifuatilia mchezo wa leo.
Kocha mkuu wa Yanga, Hans Van Der Pluijm (wa kwanza kulia) alisema wamecheza vizuri na kupoteza nafasi, lakini wanao muda wa kujisahihisha na kutetea ubingwa wao.
Mashabiki hawakuamini kama kweli wamebanwa na Azam fc
Nao mashabiki wa Azam fc walikuwa hawaamini kama kweli watafungwa, lakini wakashuhudia Kevin Friday akiwakomboa dakika ya 83 baada ya kufunga bao la kusawazisha |
Shughuli ilikuwa pevu, Azam fc walicheza kwa kujituma zaidi licha ya kuwa pungufu
Nahodha wa Yanga sc, Nadir Haroub `Canavaro` tangu aoneshe soka kubwa dhidi ya Al Ahly anawavutia zaidi mashabiki wa Yanga na kusahau maneno yao ya nyuma kwamba amezeeka
Komaa mwana tuokoe kona: Kaseja akimpa maarifa mwenzake.
Ana bahati Mbaya : Juma Kaseja alitunguliwa na Kevin Friday, hakika bao limeibua minong`ono tena.
Hapa wachezaji wa Yanga wapo makini kuzuia mpira wa kona. Hadi Hamis Kiiza baada ya kukosa penati ikabidi arudi kuzuia ili balaa lisitokee
Picha zote na Baraka Mpenja
.............................................................................
Na Baraka Mpenja Dar es salaam
0712461976 au 0764302956
AZAM FC wamefanikiwa kulinda rekodi yao ya
kutofungwa msimu huu kufuatia bao la kusawazisha la dakika za lala salama kupitia
kwa kinda wake, Kevin Friday dakika ya 83 na kulazimisha sare ya 1-1 dhidi ya mabingwa
watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara, Dar Young Africans, Uwanja wa Taifa
jijini Dar es salaam.
Kinda huyo aliyepandishwa kutoka kikosi cha pili aliitumia
vyema pasi ya kiungo fundi, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na kumchambua kipa
mkongwe Juma Kaseja na kushangilia kwa hisia kali kuashiria yeye ndiye mkombozi
wa Azam fc.
Yanga walikuwa wa kwanza kuandika bao katika dakika
ya 14 kupitia kwa Mrundi, Didier Kavumbagu aliyekutana na mpira uliorudi baada
ya kupanguliwa na kipa Aishi Salum Manula baada ya kutokea piga ni kupige
langoni mwa Azam.
Kwa matokeo ya leo, Azam fc wamefikisha pointi 44
kileleni, huku Yanga wakiendelea kusalia nafasi ya pili kwa pointi 40.
Hata hivyo Azam fc wamecheza mechi 20, wakati Yanga
leo ilikuwa mechi ya 19.
Bahati ya Yanga ilionekana kuendelea kuwepo baada ya
kupata penalti dakika ya 69 kufuatia beki Said Mourad kuunawa mpira uliopigwa na
Didier Kavumbangu, lakini Hamisi Kiiza
‘Diego’ alidakiwa penati hiyo kwa ustadi mkubwa na mlinda Mlango, Aishi Salum Manula .
Dakika 20 za mwisho, Azam fc walipata pengo la
mchezaji mmoja kufuatia beki wake wa kulia Erasto Edward Nyoni kutolewa nje kwa
kadi nyekundu kwa madai ya kutoka lugha
chafu kwa mwamuzi.
Licha ya kadi hiyo, Azam fc waliendelea kucheza kwa
kujituma zaidi wakijua wamejeruhiwa, na jitihada zao zikasababisha sare ya bao
1-1.
Kwa ujumla mchezo ulikuwa mkali na kuonesha ubora wa
vikosi vya timu zote mbili.
Baada ya mechi hiyo, kocha msaidizi wa Azam fc,
Kalimangonga Ongala alisema safari ya ubingwa bado ni ndefu kwasababu ushindani
ni mkubwa.
“Tchetche alifunga bao lilikataliwa. Kadi nyekundu
ya Erasto sijui kwanini alitolewa, kwasababu alitamka kuwa Mungu ndiye anayejua.
Sasa kuna tatizo gani hapo?”. Alihoji Kalimangonga.
Aidha, aliwapongeza vijana wake kwa kucheza soka
zuri baada ya kadi nyekundu.
“Ulikuwa mchezo mgumu kwetu. Wachezaji kuna wakati
hawakuwa watulivu. Lakini baada ya kuwa pungufu wamecheza soka la juu sana.
Tunawapongeza kwa ukomavu wao”. Alisema Kalimangonga.
Kocha huyo aliongeza kuwa sasa hesabu zao ni
kuelekea mchezo ujao dhidi ya JKT Oljoro katika uwanja wao wa Azam complex.
Naye kocha wa Yanga, Mholanza, Hans Van Der Pluijm
alisema kuwa mchezo ulikuwa mzuri, walipata nafasi hawajazitumia, hivyo
kulazimisha sare.
“Ulikuwa mchezo muhimu kwetu. Bado tuna muda wa
kujiboresha na kutetea ubingwa wetu. Najua matokeo ya leo sio mazuri kwetu,
lakini tunatakiwa kujipanga zaidi”. Alisema Pluijm.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Juma Kaseja, Juma
Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Frank Domayo,
Simon Msuva, Hassan Dilunga, Didier Kavumbangu/Mrisho Ngassa dk73, Hamisi
Kiiza/Hussein Javu dk87 na Emmanuel Okwi.
Azam FC; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Said Mourad, Kipre Balou,
Himid Mao, Salum Abubakar, John Bocco, Kipre Tchetche na Khamis Mcha/Kevin
Friday dk49.
0 comments:
Post a Comment