
.Mvua na mafuriko ni mifano hai katika baadhi ya nchi duniani
.Mapigano ya wakulima na wafugaji ni madhara ya mabadiliko ya tabianchi
Na Damas Makangale, MOblog
CHAMA CHA UMOJA WA MATAIFA CHA VIJANA (YUNA) kimesema kwamba mvua, mafuriko na mapigano ya wakulima na wafugaji yanasababishwa na mabadiliko ya tabianchi na kuomba nchi wanachama kuja na mpango mkakati wa muda mrefu kukabiliana na majanga hayo.
Akizungumza na vijana kutoka Asasi mbalimbali za vijana nchini kwenye mkutano wa kujadiliana yaliyojiri katika mkutano wa 19 wa mabadiliko ya tabianchi (COP 19) uliofanyika Warsaw, Poland Afisa Mradi wa Jukwaa la Mabadiliko ya tabianchi, Fazal Issa, amesema kwamba mabadiliko ya tabianchi yamesababisha hasara na vifo kutokana na mvua kubwa zinazosababishwa mabadiliko hayo ya tabianchi.
“kwa mantiki hiyo wanachama kutoka nchi 194 kwenye mkutano wa COP 19 nchini Warsaw, Poland walikubaliana kuja na mkakati wa muda mrefu kushughulikia mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha mvua na mafuriko sehemu nyingi duniani,” amesema.

Issa amesema kwamba moja ya makubaliano ya mabadiliko ya tabianchi ni kuja na mkakati wa teknolojia na habari ili kuweza kupiga hatua katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia teknolojia zaidi kupunguza hewa ukaa kwenye anga ya duniani.
Amesema pia kwamba katika mkutano huo wajumbe walikubaliana katika kutengeneza mfumo wa kifedha wenye kuwezesha kamati na tume mbalimbali za kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuchangisha fedha kutoka kwa wanachama mbalimbali duniani.
“mpaka sasa kamati ya utendaji wa mabadiliko ya tabianchi imeshakusanya karibu Tsh 33 billioni katika kushughulikia matatizo ya mabadiliko ya tabianchi duniani,” alilisitiza

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Asasi ya vijana ya Umoja wa Mataifa (YUNA), Dkt. Lwidiko Edward, amesema wamekuja na mkakati wa kutoa taarifa kwa vijana wenzao ya juu ya yaliojiri katika mkutano wa tabianchi na nafasi ya vijana katika kupambana na matatizo ya tabianchi duniani.
Dkt. Edward, aliongeza kuwa katika mkutano wa COP 19 vijana waliweza kushiriki kikamilifu katika kupeleka agenda zenye maslahi mapana kwa vijana na vizazi vijavyo na madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa vijana duniani.
“wanachama wa mabadiliko ya tabianchi duniani wamekubaliana kupunguza hewa ukaa ili kupunguza joto duniani kwa kuanzia ni kwenye nchi zenye viwanda vingi,” amesema.
Amesema pia mabadiliko ya tabianchi katika nchi zinazoendelea inaonekana dhahiri kwenye sehemu zenye ukame kwa sasa na mapigano ya wafugaji na wakulima ni mifano hai ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi katika nchi zinazoendelea.
Dkt. Edward, amesema kwamba kupunguza hewa ukaa duniani ni muhimu hata kama baadhi ya nchi tajiri zinategemea viwanda katika kukuza chumi zao na kuleta maendeleo kwa watu wao.


0 comments:
Post a Comment