Mboga aina ya Biringanya ikiwa shambani tayari kwa kuanza kuvunwa. Picha na Maktaba
…………………………………………………………………………
Katika siku za karibuni Wizara
ya Kilimo, Chakula na Ushirika iliwahakikishia wakulima kwa mara
nyingine tena kwamba Rais Jakaya Kikwete ametoa kauli ambayo inawaruhusu
wakulima kuwa huru katika kuuza mazao yao iwe kwa soko la ndani au nje.
Kauli hiyo imetolewa na msemaji wa wizara hiyo Richard Kasuga wakati akizungumza na gazeti hili.
“Kwa sasa wakulima wameruhusiwa
kuuza bidhaa zao kwa namna wanavyotaka katika soko wanalotaka ili mradi
wafuate sheria,” alisema Kasuga.
Wakulima hao wamesema kwamba wao
ndiyo wanaochangia asilimia 95 za gharama za kilimo inakuwaje sasa
wakati wakivuna Serikali ndiyo iwapangie wapi pa kuuza.
“Wakulima wanachangia asilimia
95 ya gharama za kilimo ….hakuna anayewasaidia kuanzia hatua za awali za
kukodi shamba, kuliandaa, kulima , kupanda, kuondoa magugu na kuvuna.
Wanafanya bila msaada lakini cha ajabu Serikali inawapangia soko, hii si
sawasawa.”
Kauli imetolewa na mmoja wa
maofisa wa Chama cha Wafanyabiashara, wenye viwanda na kilimo Peter
Lanya wakati akizungumza na Mwananchi kwenye mahojiano.
Lanya ambaye ni Makamu
Mwenyekiti (kilimo) na pia Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji
Bidhaa nje (Tanzania Exporters Association) amesema kwamba wakulima ni
vyema wakaruhusiwa kuuza bidhaa zao mahali ambapo watapata maslahi
zaidi.
Alisema kwa wakulima kazi yao
hiyo ndiyo inayowaingizia kipato ambacho hukitumia kwa ajili ya familia
na hivyo kuwanyima nafasi ya kupata kipato kizuri si sahihi.
“Ni jambo la kustaajabisha
kuwalazimisha wakulima ambao tegemeo lao la pekee la kuwapatia kipato ni
kilimo kuuza bidhaa zao katika soko ambalo halina maslahi kwao. Nadhani
ni vyema kuwaacha huru kutafuta masoko yenye maslahi,” alisema Lanya.
Kama wakulima hawataruhusiwa
kuuza kwa namna wanayoona wao inafaa, kwa vyovyote watashindwa kuwa na
kipato cha kuwasaidia kila siku na kudunduliza fedha zinazotakiwa kwa
ajili ya msimu ujao wa kilimo.
“Kama wasipopata fedha za
kutosha kwa ajili ya matumizi ya msingi ya kwao wenyewe kama matibabu
hawatakuwa na uwezo wa kufanya shughuli za kilimo kwa msimu unaofuata na
hivyo kuongeza kasi ya umaskini,” alisema Lanya.
Hata hivyo alionya wageni wanaofika nchini na kununua mazao yakiwa bado shambani kabla ya msimu wa mavuno.
“Wakati Serikali inafanya kila
liwezekanalo kuleta maendeleo ya kiuchumi , ni vyema ikawa ya kwanza
kuzuia wageni ambao hununua bidhaa zikiwa bado shambani, kabla ya muda
wa mavuno,” alisema.
Kama Serikali itachukua hatua
hiyo ya kuzuia wageni itasaidia wakulima kuwa na mavuno ya kutosha na
kujihakikishia hali bora kwao binafsi na kwa taifa.
Kwa mujibu wa Lanya, kama
Serikali inataka kuwa na uhakika wa usalama wa chakula ni vyema
ikawasaidia wakulima kupata pembejeo ili wakulima hao wafanye kazi yao
ya kulima kwa gharama nafuu.
Alisema ni dhahiri kwa kuboresha uzalishaji wa mazao utasaidia kuchangia kukua kwa pato la ndani (GDP).
“Kwa kuwa chakula hakipo katika
biashara na hivyo kuonesha kuwa mchango wake GDP ni mdogo,wakulima
wakiwezeshwa na kuwa na pembejeo,zana husika na utaalamu ni dhahiri
kwamba kipato cha GDP kitaboreshwa zaidi,” anasema Lanya.
Mawazo hayo ya Lanya yameungwa
mkono na mwenyekiti na mwanzilishi wa Chama cha Wahitimu wa Kilimo Chuo
Kikuu cha Sokoine Stephano Kingazi ambaye alisema kuwazuia wakulima
kuuza mazao yao soko la nje si kitu chema hata kidogo.
Alisema kuondolewa kwa ushindani
katika kilimo kunasababisha bidhaa kuwa na bei chini na matokeo yake
mkulima kuendelea kuwa maskini.
Hata hivyo alisema kwamba ipo haja kwa Serikali ya Tanzania kushawishi wananchi kutambua umuhimu wa kuwa na akiba ya chakula.
Alisema ni vyema kanuni zikawekwa kusaidia kuhakikisha kwamba kuna akiba ya chakula nchini.
Aidha Serikali inatakiwa
kutambua kwamba ili kuboresha hali ya upatikanaji wa chakula nchini ni
lazima kuwapatia wakulima mbegu bora. “Ukiangalia sasa utaona kwamba
mbegu nyingi zilizopo sokoni ni mbaya kuliko zile ambazo wananchi
wamezoea kuzitumia, Serikali lazima kuhakikisha wakulima wanapata mbegu
bora ili kuongeza tija” alisema Dk Kingazi.
Dk Kingazi alishauri Serikali
kutumia kila uwezekano kuhakikisha kwamba wakulima wanakwenda sambamba
na teknolojia mpya ya kilimo.
Kwa mujibu wa msemaji wa Wizara
ya Kilimo, Chakula na Ushirika Richard Kasuga pamoja na Rais Kikwete
kuruhusu wakulima kuuza bidhaa zao katika soko wanalotaka, Serikali
imechukua hatua kuboresha uzalishaji wa mazao ya chakula.
“Serikali inawekeza kwenye
miundombinu ya umwagiliaji ambapo wakulima wanaweza kutumia, kupatikana
kwa mbegu bora na kuwapatia pembejeo katika bei wanayoweza kuimudu.”
Hata hivyo msemaji huyo amekiri kwamba Serikali bado ina upungufu wa maofisa ugani.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI


0 comments:
Post a Comment