
Mheshimiwa Rais wa TFF,
Pongezi na Shukurani
1.
Naomba nianze kwa kushukuru kwa kukubali kufanyika kwa shughuli hii ya
makabidhiano ya Ofisi. Utaratibu huu haupo kikatiba wala katika kanuni
zetu, lakini ni muhimu sana kwa vile unatoa taswira ya uongozi endelevu na ushirikiano unaostahili kuwepo baina ya uongozi mpya na ule wa zamani.
2.
Aidha napenda, kwa mara nyingine, kukupongeza kwa dhati wewe binafsi
kwa kuchaguliwa kwako kuwa Rais wa Shirikisho letu pamoja na kumpongeza
Makamu wa Rais na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji kwa ushindi wao.
3.
Tumeshuhudia mchakato wa uchaguzi uliofanyika kwa uwazi, na ulio huru
na wa haki. Ninawashuru sana na kuwapongeza Wajumbe wa Kamati ya
Uchanguzi kwa ueledi na kazi nzuri
walioifanya. Kwa kiwango hicho hicho ninawapongeza na kuwashukuru
Wajumbe wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi na wa Kamati za Maadili – ngazi
ya awali na ya rufani – kwa kutekeleza wajibu wao kikamilifu na vyema
4.
Nawajibika kutoa pongezi kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kukamilisha
kazi muhimu ya kutuchagulia viongozi wetu kwa utulivu mkubwa.
5.
Utulivu wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi – kuanzia mwanzo
hadi mwisho – ni kielelezo cha ukomavu wa uongozi wa mchezo wa mpira wa
miguu nchini. Natoa shukurani za dhati kwa wanachama na wadau wote wa
mpira wa miguu nchini kwa mchango wao wa hali na mali katika kufanikisha
zoezi hili muhimu kwa mustakabali wa mpira wa miguu nchini.
Dira na Malengo ya Uongozi Uliopita
6.
Dira ya uongozi uliopita ilikuwa ni kujenga mazingira mazuri na
endelevu ya maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu nchini. Hii ilitokana
na hali ya migogoro isiyoisha na malumbano ya mara kwa mara yaliyokuwepo
kabla ya kuingia madarakani.
7.
Ili kufanikisha dira yetu, uongozi uliopita ulidhamiria kujenga
msingi bora wa uongozi wa mpira wa miguu nchini, hivyo kujiwekea
malengo yafuatayo:
· Kutengeneza
Katiba mpya na Kanuni zitakazokidhi mahitaji ya nchi yetu ya kudumisha
demokrasia na utawala bora – uwazi, uwajibikaji, na kadhalika.
· Kuhakikisha kuwa Katiba yetu na Kanuni zetu zinazingatiwa na kuheshimiwa.
· Kuweka
Kanuni za Fedha na kuchukua hatua za kujenga uaminifu katika usimamizi
wa ukusanyaji, utunzaji na matumizi ya fedha. Tuliazimia kuona hesabu
za Shirikisho zinakaguliwa na wakaguzi wenye sifa za kimataifa, na
taarifa ya ukaguzi kuwasilishwa kwenye Mkutano Mkuu kila mwaka, bila ya
kukosa.
· Kuwa
na mfumo wa mashindano utakaongeza ushindani na kuchochea uwekezaji.
Azma ilikuwa ni kuongeza idadi ya mashindano ili kutoa fursa kwa vipaji
kuonekana na kuendelezwa.
· Kuweka
jitihada katika mafunzo ya wataalamu wa mpira wa miguu nchini kwa
kuongeza idadi na kozi/semina za mafunzo ya uongozi, uamuzi, ualimu na
udaktari wa michezo.
· Kujenga
mfumo mpya wa uongozi wa timu za taifa. Lengo lilikuwa ni kuhakikisha
kuwa timu za taifa zinakuwa na uongozi wake chini ya Mwalimu/Walimu wa
timu ya taifa na kuzitofautisha na Idara ya Ufundi, pamoja na
kuhakikisha timu zetu za taifa zinashiriki michezo mingi iwezekanavyo ya
mashindano na ya kirafiki.
· Kujenga
uhusiano mzuri na wadau na washirika wetu, hususan wadau wetu wakuu
ambao ni Serikali na vyombo zake; Mashirikisho ya mpira tuliyojumuika
nayo – FIFA, CAF, na CECAFA; Wadhimini na Wafadhili wetu – kampuni,
mashirikia ya umma na watu binafsi – wanaochangia maendeleo ya mpira wa
miguu nchini kwa hali na mali.
· Kuwa
karibu na jamii na kuisaidia jamii. Nia ni kutumia umaarufu wa mchezo
wa mpira wa miguu nchini kuhamasisha maendeleo ya jamii, hasa katika
masuala ya afya ya jamii – kampeni ya malaria, ukimwi, kupambana na
madawa ya kulevya na kadhalika. Rais anayeondoka madarakani ni Balozi wa
Malaria nchini na Rais wetu mpya ni mjumbe wa Kamati ya Kitaifa ya
Kupambana na Malaria, chini ya Uenyekiti wa Waziri wetu wa Afya,
Mheshimiwa Hussein Mwinyi.
8.
Utekelezaji wa Dira tuliyojiwekea na malengo yetu ulifanyika kwa
ushirikiano wa karibu na wanachama na wadau wetu. Yaliyofanyika
yanajulikana. Itoshe kusema kuwa kazi hiyo ilifanyika kwa jitihada kubwa
na uadilifu mkubwa na kwamba malengo tuliyojiwekea yalifikiwa.
9.
Katika hotuba niliyoitoa katika Ufunguzi wa Mkutano Mkuu uliopita –
Jumamosi, tarehe 26 Oktoba 2013, niliainisha kwa kina nini kilifanyika
katika kipindi cha uongozi uliopita pamoja na mafanikio ya kazi
iliyofanyika. Napenda kuimbatanisha hotuba hiyo kama sehemu ya taarifa
hii ya makabidhiano.
10.
Matarajio yetu ni kuwa, baada ya jitihada za kuweka msingi wa uongozi
na wa maendeleo ya mpira wa miguu nchini, nguvu itaelekezwa katika
kukuza kiwango cha mpira wa miguu nchini mwetu. Tulichokifanya ni
kutayarisha Mpango wa Muda Mrefu wa Maendeleo ya Mpira Miguu Nchini – 2013 hadi 2016 (Long Term Technical Development Plan – 2013 to 2016), ambayo umeambatanishwa kama sehemu ya taarifa hii ya makabidhiano.
11.
Hivyo basi, uongozi mpya una kazi ya kusimamia na kufanikisha
utekelezaji wa Mpango huo. Pia, ni matarajio yetu kuwa uongozi mpya
utayadumisha mambo ya msingi tuliyojiwekea na kuufanyia kazi upungufu
uliopo.
Shukurani kwa Wanachama na Wadau wa TFF
12.
Pamoja na kuwa nimeshatoa shukurani mara kadhaa, napenda kwa mara
nyingine tena kuwashukuru wote waliotusaidia kufika hapa tulipo.
Nawashukuru sana wanachama wetu, wadau wetu wote – Serikali yetu na
vyombo vyake vyote, wadhamini na wafadhili, waandishi na vyombo vya
habari, wapenzi wa mpira na wananchi kwa ujumla kwa mchango wao wa hali
na mali. Bila yao tusingefika hapa tulipofika.
13.
Shukurani maalum zimwendee Mheshimiwa Rais wetu, Dk. Jakaya
Mrisho Kikwete, kwa mchango wake usiopimika. Alikuwa ni sehemu
mabadiliko haya tangu mwanzo, hata kabla ya uongozi wetu kuingia
madarakani. Ametusaidia kwa kiasi kikubwa kuzijenga timu zetu za taifa
siyo tu kwa uamuzi wake wa kulipia mishahara ya walimu wa timu ya taifa,
bali pia kwa kuwahamasisha vijana wetu kwa hali na mali wafanye vizuri.
Sina hakika kuwa yupo Rais mwingine, popote pale duniani, aliye karibu
na mapenzi ya dhati kwa vijana wa timu zake za taifa zaidi ya Rais wetu.
Zaidi ya hayo, Mheshimiwa Rais amekuwa mstari wa mbele katika
kuhamasisha utawala bora katika mpira wa miguu nchini na amefanya kila
aliloliweza kuona kuwa kiwango cha mchezo kinapanda na timu zetu
zinafanya vizuri. Napenda kutoa shukurani za dhati kwake kwa uongozi na
msaada wake.
Wanachama, Katiba na Kanuni, Wafanyakazi, Mali na Mikataba ya TFF
14. Wanachama
TFF ina jumla ya Wanachama 44 ambao wote ni wanachama hai kama ifuatavyo:
· Vyama vya Mikoa – 25
· Vyama Shiriki - 5
· Vilabu vya Ligi Kuu – 14
15. Katiba na Kanuni
Hivi
sasa TFF ina Katiba Mpya (ya Mwaka 2013) iliyofanyiwa marekebisho ya
mwisho na Mkutano Mkuu Maalum wa TFF tarehe 13 Julai 2013.
Pamoja na Katiba TFF ina kanuni zifuatazo ambazo kwa mujibu wa Katiba ya TFF hupitishwa na kamati ya Utendaji:
· Kanuni za Fedha
· Kanuni za Mashindano kuanzia Ngazi ya Wilaya hadi Ligi Kuu
· Kanuni za Utii
· Kanuni za Nidhamu
· Kanuni za Maadili
· Kanuni za Uchaguzi za Uchaguzi za TFF na za Wanachama wa TFF
· Kanuni zinazosimamia Uendeshwaji wa Bodi ya Ligi Kuu
· Kanuni
za Mashindano mengine, kama vile Copa Coca Cola, Uhai Cup, Super 8 na
Taifa Cup. Ni vyema ikafahamika kuwa kila mashindano lazima yawe na
Kanuni zinazosimamia uendeshwaji wake.
TFF
inalazimika kuzifanyia marekebisho Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wake
kufuatia marekebisho ya Kanuni za Uchaguzi za TFF. Aidha, TFF inadeni
la kutayarisha Kanuni za Chombo cha Usuluhishi (Arbitration Tribunal)
kama ilivyoainishwa katika Katiba. Hivi karibuni, TFF imepokea Kanuni za
Mfano kutoka FIFA ambayo ipo haja ya kazi hii kukamilishwa na uongozi
mpya.
16. Wafanyakazi wa TFF
Hivi sasa TFF ina jumla ya wafanyakazi 29. Kati yao yupo/wapo
· Katibu Mkuu – 1
· Wakurugenzi / Maofisa Mwandamizi – 5
· Wafanyakazi wengine – 23
Katibu
Mkuu na Wakurugenzi wapo katika kipindi cha nyongeza cha miezi sita (6)
cha mikataba yao, kinachoishia mwishoni mwa mwezi Desemba
2013. Wafanyakazi wengine wapo katika mikataba ya miaka minne yenye
kipindi cha majaribio cha miezi sita kuanzia mwanzoni mwa mwezi Septemba
2013. Hivyo basi, uongozi mpya una nafasi ya kufanya tathmini ya
mahitaji ya TFF kisha kufanya uamuzi juu ya ajira za Wafanyakazi waliopo
kadiri utakavyoona inafaa.
TFF
ilichukua hatua ya kuingia kufanya makubaliano ya hiari na wafanyakazi
wake ili kuondokana na ajira za maisha (Permanent Employment) na kubaki
na ajira za mikataba (Contract Empoyment) kwa wafanyakazi wake wote.
Wafanyakazi
wa TFF wamekuwa wakifanya kazi ngumu na saa nyingi kuliko kawaida.
Ajira ya TFF haina saa za ziada wala siku za mapumziko. Kutokana na
dhana ya kujitolea na ukweli kwamba shughuli nyingi za TFF, kama vile
michezo na mikutano hufanyika siku za mwisho wa wiki na sikukuu, ni
dhahiri kuwa Wafanyakazi wa TFF wamekuwa wakilazimika kufanya kazi siku
hizo, na mara nyingi bila malipo ya saa za ziada. Aidha, kutokana na
kukosa uwezo, uongozi uliopita ulishindwa kupandisha mishahara yao
ipasavyo.
Napenda
kuchukua nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru kwa kuihudumia TFF na
mpira wa miguu katika mazingira magumu sana. Tunauomba uongozi mpya
uliangalie suala hili kwa umakini, kama moja ya hatua za kuongeza
ufanisi wa Sekretariati.
17. Mali za TFF
Hivi sasa TFF ina mali zifuatazo:
· Kiwanja
cha Karume Stadium, chenye hati namba 27026 iliyotolewa tarehe 10
Novemba 1981. Kiwanja cha Karume kina ukubwa wa ekari 8.26. Ombi la
kuingezea muda hati hiyo limeshapelekwa na linafuatiliwa.
· Ndani
ya Kiwanja hicho, kuna Jengo la ofisi ya TFF, Jengo la Kituo cha Ufundi
(Technical Centre) na Uwanja wa nyasi za bandia wa Karume.
· Kiwanja
cha Tanga chenye ukubwa wa hekta 7.6 (ekari 19) kilichopo katika eneo
zuri sana mjini Tanga. Kiwanja hiki tayari kimeshalipiwa na hivi sasa
taratibu zinaendelea kukamilisha taratibu za kukiandikisha na kupata
hati.
· Magari
sita (6) na Trekta moja (la kusafishia uwanja wa nyasi bandia). Magari
hayo ni: Bus kubwa aina ya Yutong, basi dogo aina ya Coaster, magari ya
aina 4WD Ford Everest, Rav 4, Suzuki Escudo na Honda CVR. Mawili kati
magari hayo – Suzuki Escudo na Honda CVR – yanatumika lakini hayapo
katika hali nzuri. Ni vyema uongozi mpya ukayafanyia tathmini magari
hayo na kufanya maamuzi muafaka kadiri utakavyoona inafaa.
· Fedha
taslimu Shilingi 33,518,000 na US$ 1,390 zipo katika akaunti hivi sasa.
Hii ni baada ya TFF kufanya malipo ya Shilingi 158,000,000 kwa ajili ya
Mkutano Mkuu (uliofanyika wiki iliyopita) na malipo ya Shilingi
56,240,000 yaliyofanyika kwa ajili matayarisho ya Timu ya Taifa ya
Wanawake U-20 na gharama za mchezo baina ya timu yetu ya Taifa na ile ya
Msumbiji uliofanyika wiki iliyopita. Hata hivyo, leo hii US$ 415,000
(Shilingi 664,000,000) kimehamishwa kutoka kwenye Akaunti za TBL kwenda
kwenye Akaunti za TFF. Fedha hizo zitakuwa tayari kwenye Akaunti ya TFF
ifikapo Jumanne wiki ijayo. Malipo haya yalikuwa yafanyike karibu miezi
miwili iliyopita lakini yalicheleweshwa ili kutoa nafasi kwa zoezi la
ukaguzi wa fedha za udhamini wa TBL kufanyika. Zoezi limefanyika vyema
na kufikia ukingoni, ndiyo maana malipo yamefanyika. Malipo mengine
yanayofanana na hayo, ya US$ 420,000 (Shilingi 672,000,000) yanatarajiwa
kufanyika wiki mbili kutoka sasa – katikati ya mwezi huu wa Novemba
2013.
Hivyo
basi, uongozi unaoingia madarakani hautaanza kwa shida. Ni matarajio
yetu kuwa hatua ya awali itakuwa kurejesha fedha kwenye akaunti
zilikoazimwa kinachofikia US$ 166,509 – US$ 148,174 kutoka kwenya
Akaunti za FAP na US$ 18,335 kutoka kwenye Akaunti ya TRA – kwa ajili ya
kugharimia Mkutano Mkuu na matumizi ya Taifa Stars kwa ajili ya
matayarisho na safari ya kwenda Gambia.
Ili
kujiridhisha kuwa fedha za udhamini zinatumika kama ilivyokubalika
katika mikataba, TFF imetoa nafasi kwa wadhamini kufanya ukaguzi wa
fedha inazozitoa wakati wowote ule. Utamaduni huu tumekuwa nao katika
kipindi chote cha utawala wa uongozi wetu, ili kutoa imani kwa wadhamini
na kuhakikisha kuwa malengo ya udhamini husika yanafanikiwa. Huu ni
utaratibu mzuri na ni matumaini yetu kuwa utadumishwa.
Jengo
la Kituo cha Ufundi ndiyo kwa limekamilika kukarabatiwa na bado
halijafunguliwa rasmi. Ukarabati huo umefanikisha kutengenezwa kwa mfumo
wa maji machafu unaojitegemea. Hivyo, kutohitaji kutengemea mashimo ya
Jengo la Ofisi za TFF. Hatuo ya mwisho ya kazi hiyo ni kukamilisha
ukaguzi wa matumizi yaliyofanyika katika ukarabati huo na kuiwasilisha
CAF mapema iwezekanavyo. Hayo ndiyo makubaliana kuhusiana na msaada
uliotolewa na CAF – unaojulikana kama CAF FAP 2.
Ukarabati
wa Kituo cha Ufundi umefanywa, pamoja na sababu nyingine, ili kutoa
fursa kwa Mradi wa Ujenzi wa Karume kuendelea. Kama nilivyoeleza katika
Mkutano Mkuu, dhamira ni kuwekeza katika Mradi wa Ujenzi wa jengo /
majengo yenye hadhi kubwa kwa ajili ya kukodishwa kuzunguka uwanja huo.
Jengo lililo karabatiwa na uwanja wa mpira vitabaki na kuendelea
kutumiwa kama Kituo cha Mafunzo. Jambo la muhimu ni kuhakikisha kuwa
uwekezaji katika mradi huo hauhitaji dhamana ya uwanja wetu na majengo
yetu. Ni imani yetu kuwa njia muafaka inapatikana, ikiwa ni pamoja na
utaratibu wa ‘Build, Operate and Transfer’ (BOT).
18. Hesabu za TFF
Ripoti
ya Ukaguzi wa hesabu za TFF hadi kufikia Desemba 2012 iliwasilishwa
katika Mkutano Mkuu uliopita. TFF ilipata Hati Safi ya Ukaguzi wa hesabu
zake na Mkutano Mkuu ukaikubali na kuipitisha ripoti hiyo hesabu za
mwaka 2012. Aidha, taarifa ya hesabu za TFF kwa kipindi cha kuanzia
tarehe 1 Januari hadi 30 Septemba 2013 kusambazwa kwa Wajumbe wa Mkutano
Mkuu.
Ifahamike
kuwa TFF imekuwa ikipata Hati Safi, kila mwaka katika kipindi cha miaka
minane iliyopita. Hatuna shaka kuwa hali hii itaendelea.
19. Mikataba ya Udhamini
TFF inayo mikataba ifuatayo ya udhamini na Wadhamini wafuatayo:
· Vodacom – Udhamini wa Ligi Kuu
· TBL – Taifa Stars
· Coca Cola – Mashindano ya Copa Coca Cola
· SSB & Co – Mashindano ya Uhai
· Bank ABC – Super 8
· Azam Media – Haki za Matangazo ya Television kwa Ligi Kuu
Aidha,
baadhi ya vilabu kama vile Yanga na Simba vinadhaminiwa na TBL,
Coastal Union inafadhiliwa na Tanga Cement na Azam FC inadhaminiwa na
Azam Cola.
Changamoto zinazoikabili TFF
20.
Zipo changamoto nyingi zinazoikabili TFF lakini kubwa kwa
maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu na ambazo uongozi mpya hauna budi
kuzishughulikia ni ulazima wa:
· Kuendeleza
sola la vijana na watoto kwa kutoa fursa kwa watoto/vijana wengi kupata
malezi mazuri ya uchezaji wa mpira wa miguu ili kupanua wigo wa kupata
wachezaji wenye vipaji. Katika jambo hili bado tuko nyuma sana.
Tulididimia sana kutokana na kufutwa kwa michezo mashuleni. Ipo haja ya
uongozi mpya kushirikiana na Serikali kuhamisha michezo shuleni, kama
hatua ya wali ya kutatua tatizo la soka la vijana/watoto.
· Kuendeleza
soka la wanawake. Matatizo ya soka la wanawake yanafanana na ya soka la
vijana. Tofauti ni ndogo sana. Kama ilivyo kwa soka la vijana, hatua
muhimu kufanyika kwa jitihada ya kuwahamasisha wasichana wacheze mpira
wa miguu shuleni
· Kuhakikisha
ueledi unazingatiwa katika uongozi wa Vilabu na Vyama Wanachama wa TFF.
Kinyume chake hatutaweza kushindana na wenzetu ambao walishapiga hatua
katika taaluma ya uongozi wa michezo. Vilabu vyetu ni lazima
vihakikishe kuwa vinatimiza masharti ya ‘Club Licencing’ kama
yalivyotolewa na CAF, pamoja na marekebisho yake. Huu ni mtihani kwetu.
Ni lazima tufaulu kutimiza masharti hayo, vinginevyo tutabaki nyuma. Ipo
haja ya kuuangalia kwa mfumo wa uongozi wa Vilabu vyetu na Vyama Vyetu
kwa azma ya kubuni mfumo utakaotuletea ufanisi zaidi wa kiungozi na
uendeshaji kuliko ilivyo hivi sasa.
· Kuhamasisha
uwekezaji katika maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu nchini. Tuna
upungufu mkubwa wa vifaa na viwanja vya kuchezea. Ni vigumu kuundeleza
mchezo wa mpira bila ya kuwa na viwanja vya kuchezea na vifaa. Aidha,
zinahitajika raslimali watu na fedha katika kulea na kuwaendeleza
wachezaji na wataalamu wetu. Licha ya hapo kiasi kikubwa cha fedha
kinahitajika kwa ajili ya matumizi mengine ili timu ifanye vizuri. Kwa
maneno mengine tunahitaji kufanya kila jitihada kuhamasisha watu
binafsi, makampuni na Serikali iwekeze katika mpira, wadhamini zaidi
wajitokeze na wapenzi wengi zaidi wachangie timu zao – kwa njia
mbalimbali – ili kuongeza mapato ya vilabu na vyama husika. Vilabu vyetu
na Vyama Wanachama wa TFF vinakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha za
uendeshaji. Mawazo au fikra kuwa kuna fedha nyingi katika mpira wa
miguu ni dhana isiyo na msingi na inayotokana na kutofahamu gharama za
uendeshaji wa vilabu na vyama vyetu. Pamoja na ongezeko kubwa la mapato
ya milangoni na mchango wa udhamini katika kipindi cha uongozi uliopita,
bado kinachopatikana hakikidhi hata theluthi moja ya mahitaji muhimu.
Haja ya kuongeza mapato ndiyo changamoto mama. Ikitatuliwa itasaidia kwa
kiasi kikubwa kupunguza makali ya changamoto nyingine.
· Ili
kuvutia uwekezaji, udhamini na misaada kwenye mpira wa miguu, ni lazima
tuhakikishe kuwa tunaendelea na jitihada za kujenga uaminifu wa
utunzaji na matumizi ya fedha ndani ya TFF. Ipo haja ya kuhakikisha kuwa
Kanuni za Fedha zinazingatiwa na hesabu zetu zinakaguliwa mara kwa
mara. Mpango wa Tiketi za Elektroniki ni muhimu usimamiwe kwa nguvu zote
kwa vile sio tu utatuongezea mapato bali pia utatoa picha ya uaminifu
na ueledi.
Uhusiano na ZFA
21.
TFF haina budi kufanya kila linalowezekana kudumisha uhusino mzuri
baina yake na ZFA. TFF inatambulika na FIFA kama msimamizi wa mchezo wa
mpira wa miguu nchini Tanzania. Lakini ukweli ni kuwa mchezo wa mpira
katika visiwa vya Unguja na Pemba unasimamiwa na ZFA. Hakuna matarajio
ya hali hiyo kubadilika. Kwa sababu hiyo, upo ulazima wa kudumisha
uhusiano uliopo na kuhakikisha kuwa ZFA inapata haki ya kupewa baadhi ya
miradi inayotokana na fedha za FIFA – FAP. Kwa vile fedha hizo hatolewa
kwa njia ya miradi, utaratibu tuliokubaliana ni kuhakikisha kuwa kila
mwaka baadhi ya miradi / semina zinafanyika visiwani.
Wakaguzi wa Hesabu za TFF
22. Hesabu za TFF zinakaguliwa makampuni ya Ukaguzi wa Hesabu yafuatayo:
· TAC Associates – kwa hesabu zote za TFF
· KPMG – kwa fedha za FIFA
Bodi ya Wadhamini
23.
Mkutano Mkuu wa Mwaka 2011 uliridhia kuundwa kwa Bodi ya
Wadhamini wa TFF na Mkutano Mkuu uliopita ulipitisha majina ya Wajumbe
wa Bodi ya Udhamini kama ifuatavyo:
· Said El Maamry – Mwenyekiti
· Mh. Joel Bendera – Makamu Mwenyekiti
· Dr. Ramadhani Dau – Mjumbe
· Steven Mashishanga – Mjumbe
· Mohamed Abdulaziz – Mjumbe
Mheshimiwa Rais,
napenda kukubidhi taarifa hii ya makabidhiano leo hii tarehe 2 Novemba
2013 kwa ufahamu na kumbukumbu za TFF. Tafadhali jisikie huru kuomba
ufafanuzi wa jambo lolote lililomo katika taarifa hii au kuomba taarifa
juu ya jambo ambalo kwa bahati mbaya limesahauliwa. Sekretariati ya TFF inawajibika kutoa ufafanuzi unaohitajika.
Tunakutakia wewe
mwenyewe na uongozi wako kila la heri na mafanikio katika kuingoza wa
TFF kuelekea kule kunakotarajiwa na wapenzi wa mpira wa miguu nchini.
Wadau na wapenzi wote wa mpira wa miguu wanaoitakia heri nchi yetu wapo
nyuma yako.
Leodegar Tenga Angetile Osiah
RAIS WA TFF KATIBU MKUU WA TFF
0 comments:
Post a Comment