![]() |
|
Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) |
MECHI YA TANZANITE SASA KUCHEZWA DAR
Mechi
ya kwanza ya raundi ya michuano ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika kwa
wanawake chini ya miaka 20 kati ya Tanzania (Tanzanite) na Afrika Kusini
iliyokuwa ichezwe Mwanza sasa itafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Baada
ya ukaguzi uliofanywa na maofisa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), imebainika uwanja huo unatakiwa ufanyiwe marekebisho
ambayo hayawezi kuwahi Desemba 7 mwaka huu, siku ambayo ndiyo mechi hiyo
inatakiwa kuchezwa.
Vyumba vya wachezaji vya uwanja huo ndilo eneo ambalo linatakiwa kufanyiwa marekebisho makubwa.
KILIMANJARO STARS YATUA SALAMA NAIROBI
Timu
ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) imewasili salama Nairobi, Kenya
tayari kwa mashindano ya Kombe la Chalenji yanayoanza kesho (Novemba 27
mwaka huu) katika Uwanja wa Nyayo.
Kilimanjaro
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iliwasili saa 3 usiku
kwa ndege ya RwandAir, na imefikia katika hoteli ya Sandton iliyoko
katikati ya Jiji la Nairobi.
Kwa
mujibu wa programu ya Kocha Mkuu Kim Poulsen, Kilimanjaro Stars leo
(Novemba 26 mwaka huu) ni mapumziko ambapo kesho itafanya mazoezi
kujiandaa kwa mechi yake ya kwanza dhidi ya Zambia itakayochezwa Novemba
28 mwaka huu Uwanja wa Machakos.
WANNE WASHINDA UCHAGUZI CECAFA
Baraza
la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limepata
wajumbe wapya wa wanne wa Kamati ya Utendaji katika uchaguzi uliofanya
leo (Novemba 26 mwaka huu) hoteli ya Hillpark jijini Nairobi.
Uchaguzi
huo ulifuatiwa na Mkutano Mkuu wa CECAFA ulioongozwa na Mwenyekiti wake
Leodegar Tenga na kuhudhuriwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Kalusha Bwalya na ofisa wa
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Emmanuel Maradas.
Rais
wa zamani wa Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA),
Lawrence Mulindwa ndiye aliyeongoza katika uchaguzi huo ambapo
wasimamizi walikuwa Bwalya na Maradas.
Mulindwa
alipata kura zote 12 na kufuatiwa na Tariq Atta wa Sudan (10),
Abdigaani Saeb Arab wa Somalia (9) na Raoul Gisanura wa Rwanda (8).
Atta, Arab na Gisanura walikuwa wakitetea nafasi zao.
Walioshindwa
ni Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Sudan Kusini (SSFA), Alei Chabor
aliyepata kura tano na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya
(FKF), Sam Nyamweya aliyepata kura nne.
MICHUANO YA UHAI YAHAMIA CHAMAZI
Michuano
ya Kombe la Uhai imeingia hatua ya robo fainali ambapo sasa mechi
zinachezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, nje kidogo ya
Jiji la Dar es Salaam.
Uamuzi wa kuhamisha mechi hizo kutoka viwanja vya Karume na DUCE ni kuziwezesha zote kuoneshwa moja kwa moja (live) na Azam Tv.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tunaomba radhi kwa washabiki ambao watakuwa wameathirika kutokana na uamuzi huo.
USAJILI DIRISHA DOGO KUFUNGWA DESEMBA 15
Wakati
dirisha dogo la usajili linafungwa Desemba 15 mwaka huu, Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tunazikumbusha klabu zote kuheshimu kanuni
na kuzingatia muda uliowekwa.
Pia
tunakumbusha kuwa kupeleka mchezaji kwa mkopo katika klabu nyingine
hakutoi nafasi ya kusajili mchezaji mpya. Kama klabu ilisaji wachezaji
30 maana yake ni kuwa haina nafasi ya kuongeza wachezaji.
Kwa
upande wa wachezaji wa kigeni (foreign players), tunakumbusha kuwa
kuanzia msimu ujao 2014/2015 watakuwa watatu tu badala ya watano wa
sasa.
Kuhusu
usajili wa wachezaji kutoka nje mpaka sasa hakuna hata klabu moja
imeshaingia kwenye TMS kuomba uhamisho. Itakapofika Desemba 15, system
ya TMS itafunga.
RAMBIRAMBI MSIMBA WA ANDREW KILOYI
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za
kifo cha mwamuzi wa zamani wa FIFA, Andrew Kiloyi kilichotokea mjini
Iringa.
Kwa
mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Mkoa wa
Iringa, Ramadhan Mahano, Kiloyi alifariki dunia juzi (Novemba 24 mwaka
huu) kutoka na ugonjwa wa fangasi ya ubongo, na marehemu amesafirishwa
kwenda kwao Kigoma ambapo atazikwa.
Kiloyi
alizaliwa Mei 5, 1968. Alijiunga na uamuzi wa mpira wa miguu mwaka 1988
ambapo alipata beji ya FIFA mwaka 2001 akiwa mwamuzi msaidizi.
Alistaafu uamuzi mwaka 2009, na hadi anafariki akiwa mjumbe wa Kamati ya
Waamuzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa (IREFA).
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pole kwa familia ya marehemu,
IREFA, ndugu, jamaa na marafiki kutokana na msiba huo na kuwataka kuwa
na moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hicho cha majonzi. Mungu
aiweka mahali pema roho ya marehemu Kiloyi.
Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)


0 comments:
Post a Comment