Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,Bernard Membe
akimsindikiza mgeni wake Waziri mwenza wa Kenya, Amina Mohammed baada
ya waziri huyo kumaliza kuzungumza na waandishi wa habari Dar Salaam.
PICHA|EMMANUEL HERMAN
Bila
shaka hakuna Mtanzania hata mmoja ambaye hakuipongeza hatua ya Serikali
ya Kenya kutuma ujumbe wa kuunga mkono msimamo wa Tanzania wa kutojitoa
katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), licha ya nchi za Uganda, Kenya
na Rwanda kufanya mikutano kujadili mipango na masuala yanayohusu
jumuiya hiyo pasipo kuihusisha Tanzania, kinyume kabisa na Mkataba wa
Jumuiya hiyo.
Tanzania ilipinga kwa nguvu zote
hatua ya nchi hizo kuitenga hata katika masuala yaliyo chini ya jumuiya
hiyo, ambayo kwa mujibu wa mkataba huo yanapaswa kujadiliwa na
kutekelezwa kwa pamoja na nchi zote wanachama. Rais Jakaya Kikwete
alilazimika kulihutubia Bunge wiki iliyopita na kuelezea kwa kirefu
ukiukwaji wa mkataba huo na athari za kuzitenga Burundi na Tanzania
katika mikutano inayojadili masuala ya EAC.
Pamoja na kuzikosoa na kuzilaumu
vikali nchi hizo tatu kwa kukiuka mkataba huo pamoja na itifaki zake
mbalimbali, Rais Kikwete aliweka wazi msimamo kwamba Tanzania kamwe
haitajitoa katika Jumuiya hiyo na itaendelea kuwa mshirika mwaminifu wa
Jumuiya hiyo pasipo kutetereka. Msimamo huo bila shaka uliondoa hofu
iliyokuwa imetanda miongoni mwa wananchi katika nchi zote wanachama wa
EAC, kwamba Tanzania ingejitoa katika Jumuiya hiyo kutokana na kutengwa
na nchi hizo tatu zilizokuwa zikiunda kile kilichoitwa ‘Coalition of the
willing’ (Ushirikiano wa wenye hiari).
Hotuba ya Rais Kikwete
ilifikisha ujumbe kule kulikotarajiwa. Ikiwa ni siku nne baada ya Rais
kulihutubia Bunge akilalamikia nchi hizo kuitenga Tanzania, Kenya
imemtuma Waziri wake wa Mambo ya Nje, Amina Mohamed kuja hapa nchini
kuwasilisha ujumbe wa Rais Uhuru Kenyatta kwamba nchi yake iko tayari
kushirikiana na Tanzania kwa kutambua umuhimu wake kama moja ya
waanzilishi wa Jumuiya hiyo. Waziri huyo alisema kuwa, kuja kwake hapa
nchini kunafuatia Serikali ya Kenya kusoma kwa undani hotuba ya Rais
Kikwete ambayo alisema, ilikuwa nzuri na ilitolewa kwa nia njema tu ya
kuimarisha Jumuiya hiyo na siyo kuidhoofisha.
Sisi tunadhani hatua ya Kenya ya
kutafuta maridhiano na Tanzania ni ya kupongeza, hasa tukitilia maanani
ukweli kwamba moja ya sababu kubwa zilizosababisha kuvunjika kwa EAC
mwaka 1977 ilikuwa ni kutokuwapo utamaduni wa nchi wanachama kujikosoa
na kuona umuhimu wa kumaliza tofauti zao kwa njia ya mazungumzo. Hatua
hiyo ya Kenya yafaa iwe mfano kwa nchi nyingine ndani ya Jumuiya hiyo,
kwamba zijisahihishe pale zinapojiridhisha kwamba zimekosea hapa au
pale.
Hapa hatuna maana kwamba
Tanzania haikuchangia lolote katika kufikiwa kwa hali hiyo ya kutengwa.
Kwa mfano, mbali na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi imekuwa
ikilalamikiwa na nchi nyingi jirani zinazotumia Bandari ya Dar es
Salaam. Yamekuwapo malalamiko mengi na ya muda mrefu kuhusu
ucheleweshaji wa kupakua na kupakia shehena za mizigo, ukubwa wa tozo za
bandari na barabara pamoja na uchakachuaji wa mafuta. Ndiyo maana
baadhi ya nchi hizo zimeamua kutumia Bandari ya Mombasa.
Ni
matumaini yetu kwamba nchi wanachama wa EAC zitachukulia mvutano
uliokuwapo kati yao na Tanzania kama changamoto ya kuzisukuma
kushirikiana zaidi ili kujenga Jumuiya yenye nguvu kubwa kiuchumi.
Wakati huohuo, hatua hiyo ya Kenya ni ya kijasiri, siyo udhaifu.
CHANZO: MWANANCHI


0 comments:
Post a Comment