Hatimaye mabingwa wa ligi soka kuu Tanzania bara, Dar Young Africans wamemaliza ziara yao ya mikoani kwa kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya maafande wa Rhino Rangers katia dimba la Ali Hassan Mwinyi jioni ya leo na kutoka suluhu pacha ya bila kufungana.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka mkoani Tabora, Afisa habari wa klabu ya Yanga, Baraka Kizuguto alisema mchezo wa leo ulikuwa mzuri japokuwa kwa kiasi fulani waamuzi wameshindwa kuchezesha kwa uzuri.
“Kuna bao lilifungwa na John Tegete, lakini muamuzi alikataa, sawa sio mbaya, timu imecheza vizuri sana, cha kusikitisha ni hali halisi ilivyokuwa uwanjani, mashabiki walijazana nyuma ya benchi la ufundi la klabu yetu, tukiwaambia watoke walikuwa wanagoma, huo ni ushamba katika soka”. Alisema Kizuguto.
Afisa habari huyo alisema timu yao ilipata nafasi nyingi za kufunga, lakini walishindwa kuzitumia vizuri. Pia amelalamikia hali mbovi ya uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.
Kizuguto alisema katika mchezo wa leo kikosi cha Yanga kilitulia na kupiga soka safi, lakini mazingira halisi ya uwanjani na waamuzi yamewanyima ushindi, lakini sio kesi kwao kwani ilikuwa mechi ya kirafiki.
“Baada ya mchezo wa leo, kesho timu inasafiri kuelekea jijini Dar es salaam kuendelea na michakato mingine ya mazoezi, tunawaomba mashabiki wetu na watanzania kwa ujumla kutuombea safari njema”. Alisema Kizuguto.
Katika ziara yao hiyo ya mikoani, Yanga wameshindwa kupata ushindi katika michezo yao mitatu waliyocheza. Walitoka sare ya 1-1 na KCC ya Uganda katika dimba la CCM Kirumba, walifungwa mabao 2-1 na KCC uwanja wa Kambarage mjijini Shinyanga na leo hii wamemaliza mpango mzima kwa kutoka suluhu na Rhino Rangers.
Yanga baada ya kurejea Dar, itacheza mechi mbili za kujipima uwezo na URA ya Uganda ambao watakuwepo nchini kufanya ziara ya maandalizi ya ligi kuu ya nchini mwao, na wakiwa nchini watacheza dhidi ya Simba na Yanga, pamoja na timu nyingine watakazopangiwa.
Yanga baada ya kutwaa ubingwa msimu uliopita na kuwapokonya watani wao wa jadi, Simba SC, sasa wana kibarua kikubwa cha kuandaa timu kwa ajili ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika mwakani. Wenzao Simba wanaujua moto wake baada ya kutolewa nishai na Libolo ya Angola kwa kipigo cha nje ndani cha mabao 5-0.
0 comments:
Post a Comment