
Na Baraka Mpenja
Kwa wale ambao hawalijui vizuri jiji la Mbeya, ukisikia uwanja wa chuo cha magereza Kiwira si mchezo, hilo ndilo chimbo la maafande wa Tanzania Prisons “Wajelajele” kunoa makali yao wanaposhiriki michuano mbalimbali hususani ligi kuu soka Tanzania bara.
Tayari wanagwaride hao wameshatia miguu yao Kiwira na kuweka kambi ya kujiandaa na mitanange ya ligi kuu huku wakitamba kurejesha makali yao ya miaka ya nyuma.
Kwa wafuatiliji wazuri wa soka la Bongo, lazima wanakumbuka Prisoms ile ya Juma Mwambusi iliyocheza kombe la shirikisho barani Afrika, moto wake ulikuwa mkali sana, na sasa hivi wanatamba kurudi katika kiwango kile.
Akizungumza na MATUKIO DUNAINI kwa njia ya simu kutoka Kiwira, katibu mkuu au mtendaji mkuu wa shughuli za kila siku za klabu hiyo, Sadick Jumbe amesema kikosi kizima kipo kambini na morali ya wachezaji ni kubwa , huku kocha wao mkuu Jumanne Chale akiwapatia mbinu mpya za kung`ara msimu ujao.
Jumbe alisema kabla ya kwenda Kiwira walikuwa wanaendelea na mazoezi katika dimba la Sokoine mjini Mbeya, lakini baada ya ratiba kuwekwa hadharani , wameshawasili maeneo yao ya kujichimbia na kupiga jalamba la nguvu.
“Tulikuwepo Mbeya mjini ambapo wachezaji walikuwa wanaendelea na mazoezi, lakini kwa saa tupo chimbo Kiwira, maeneo haya ni mazuri sana kwetu. Hakika nakwambia ndugu yangu, msimu ujao lazima tuwang`ang`anie watu katika nafasi tatu za juu hasa Wakongwe Simba na Yanga”. Alisema Jumbe.
Katibu huyo alisisitiza kuwa kwa sasa jiji la Mbeya limepata timu mbili, lakini mashabiki wasigawanyike sana wakati timu zao zinacheza na timu pinzani, bali watangulize uzalendo.
“Nakumbuka mwishoni mwa msimu uliopita, mashabiki na wadau wa soka jijini Mbeya walijitolea kufa na kupona kuinusuru timu isishuke daraja, jitihada zao zilizaa matunda, moyo ule walioonesha wakati ule, tunawaomba waendelee kutuonesha pamoja na ndugu zetu wa Mbeya City”. Alisema Jumbe.
Jumbe aliongeza kuwa katika historia ya soka, mkoa wa Mbeya una heshima kubwa sana kutokana na klabu za zamani wakiwemo mabingwa wa mwaka 1986 wa ligi kuu Tanzania, “Banyambala” Tukuyu Stars, Meco, Sigara na nyinginezo, hivyo wao na Mbeya City watajitahidi kurudisha mkoa huo katika ramani ya soka la Tanzania.
0 comments:
Post a Comment