Na Baraka Mpenja
Ligi kuu soka Tanzania bara imeendelea kushika kasi kwa mechi tatu kupigwa katika miji ya Tanga, Morogoro na Kagera.
Uwanja
wa CCM mkwakwani jijini Tanga vinara wa ligi hiyo Yanga wamepunguzwa
kasi baada ya kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya maafande wa
Mgambo JKT.
Bao
la Mgambo limefungwa dakika ya 37 kipindi cha kwanza kupitia kwa nyota
wake Fulljelly Maganga wakati kwa upande wa Yanga wamesawazisha dakika
ya 87 kupitia kwa winga mwenye kasi kubwa Simon Msuva .
Baada
ya Mchezo huo kumalizika katibu mkuu wa Mgambo, Antony Mgaya alisema
mechi ilikuwa ngumu lakini wamecheza vizuri na kuwahimili wapinzania wao
waliojaa sifa kwenye vyombo vya habari.
“Yanga
ni timu ya kawaida sana, wamecheza soka la kawaida na kama tusingefanya
makosa dakika za lala salama walikuwa wameshatolewa nishai”. Alisema
Kwa
upande wa Yanga kupitia kwa afisa habari wake Baraka Kizuguto walisema
mwamuzi amechezesha chini ya kiwango na kuharibu ladha ya soka CCM
Mkwakwani.
“Hakika
kuna mambo ya ajabu, mwamuzi kachezesha ovyo kweli, kawabeba Mgambo,
lakini sisi tunajipanga kwa mchezo ujao dhidi ya JKT Ruvu ambao lazima
tuwafunge halafu tujitangazie ubingwa msimu huu”. Alisema Kizuguto.
Huko
mashamba ya miwa Manungu Turiani Mkoani Morogoro, watengeneza sukari wa
Mtibwa sugar wameshuka dimbani dhidi ya maafande wa JKT Oljoro na
kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Bao la Mtibwa limefungwa kupitia kwa kiungo wake Twaa Ally dakika ya 37 ya kipindi cha kwanza.
Msemaji wa klabu hiyo Tobias Kifaru Lugalambwike alisema mchezo huo ulikuwa wa kusisimua kutokana na uwezo wa wapinzani wao.
“Tunajipanga
dhidi ya Lyon watakaokuja nyumbani mchezo ujao, tunajipanga kupata
ushindi na vijana wetu wapo katika morali kubwa sana”. Alisema Kifaru.
Mchezo
mwingine umepigwa katika dimba la kaitaba Mkoani Kagera baina ya
wenyeji wa uwanja huo vijana wa Abdallah Kibadeni “King Mputa”, Kagera
Sugar dhidi ya vijana wa mitaa ya kishamapanda jijini Mwanza Toto
Africa wanaonolewa na kocha John Tegete.
Kibaden
alizungumza na mtandao huu na kutujuza matokeo kuwa wameibuka na
ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Toto na kujisimika zaidi nafasi ya tatu ya
ligi hiyo.
“Toto
wamecheza vizuri na kama wangekuwa wanacheza hivi siku zote hakika
wasingekuwa hapa walipo, lakini sisi tulijipanga zaidi na ndio maana
tumewafunga nyumbani”. Alijigamba Kibaden.
Baada
ya michezo hiyo Yanga bado wapo kileleni wakijikusanyia pointi 53
kibindoni na kuchanja mbuga kuelekea ubingwa wa ligi kuu msimu huu
unaomilikiwa na watani zao wa jadi klabu ya simba ya Dar es salaam
“Taifa Kubwa”, nafasi ya pili wapo Azam wenye poiti 47, Kagera wapo
nafasi ya tatu wakiwa na pointi 40 huku Simba wakibaki nafasi ya nne na
pointi zao 36 kibindoni.
0 comments:
Post a Comment