![]() |
MBWANA MAKATA |
Kufuatia
malalamiko mengi juu ya waamuzi wakati huu wa ngwe ya lala salama ya
ligi kuu soka Tanzania bara, shirikisho la kandanda Tanzania
limeshauriwa kufanyia uchunguzi suala hilo ili kujua hali halisi ya
jambo hilo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na FULLSHANGWE,
aliyekuwa kocha wa maafande wa JKT Oljoro siku za hivi karibuni Mbwana
Makata, alisema malalamiko siku zote yanaweza kuwa ya kweli au uzushi
tu, lakini TFF wanatakiwa kufanyia kazi kwa uangalifu mkubwa.
“TFF
kupitia kamati zake wanatakiwa kufumbua macho juu ya jambo hili, ligi
inafikia ukingoni na kuna lawama nyingi kwa waamuzi, kinachoatakiwa
kufanyika ni kukaa chini na kuunda kamati za kuchunguza suala hilo ili
haki itendeke”. Alisema Makata.
Makata
aliongeza kuwa ligi inafikia ukingoni, ushindani ni mkubwa sana
hususani kwa timu zinazopigana kufa na kupona kukwepa mkasi wa kushuka
daraja msimu huu hivyo kuna haja ya kuiangalia kwa jicho la darubini na
kubaini udanganyifu uliopo.
Kocha
huyo mwenye historia ya kucheza soka na kufundisha timu nyingi
alisisitiza kuwa kwa sasa kuna kamati zinazoundwa kisiasa kwa madai kuwa
zinasaidia timu zao zisishuke daraja, lakini kamati hizi zinatia
mashaka kutokana na kuundwa wakati ligi inafikia ukiongoni.
“Mimi
nashangaa sana, nasikia viongozi wa serikali wanajiingiza kuunda kamati
za kusaidia timu isishuke daraja, kama kweli wana nia ya kuisaidia timu
kwanini wasingejitokeze mapema?, timu ina hali mbaya ndio wanakuja
kuisaidia, hapa ndipo wasiwasi unaibuka”. Alisema Makata.
Makata
aliwata viongozi wanaojitokeza kusaidia timu wakati mambo yamekuwa
magumu kuacha tabia hii na kama lengo lao ni hilo basi wajitokeze
mwanzoni mwa msimu wakati timu inajiandaa kuanza michuano ya ligi na si
ngwe ya lala kwa buriani .
Akizungumzia
hali halisi ya ligi yetu, Makata alisema ligi ina ushindani mkubwa sana
lakini kuna ulazima wa TFF na wadhamini wa ligi kubadili mfumo wa
utoaji wa zawadi.
“Wajitahidi
kutoa zawadi kwa timu zote zinazosalia ligi kuu, hii itapelekea timu
kushindana kupata zawadi za nafasi nyingine mbali na nafasi ya kwanza,
ikiwa hivi ligi itakuwa ya kuvutia sana”. Alishauri Makata.
Pia Makata imezishauri timu kushindani hadi dakika ya mwisho hata kama zina uhakika wa kubakia ligi kuu.
Makata
ni mchezaji wa zamani wa timu ya Waziri Mkuu Dodoma miaka ya sabini na
themanini, Tukuyu stars “Banyambala” miaka ya themanini na Dar Young
Africans miaka ya themanini na tisini.
Baada
ya hapo alianza ukocha mwaka 1999 na klabu ya Mji Mpwapwa ya Dodoma
aliyoipandisha daraja, Twiga ya Kinondoni ambayo baadaye ilinunuliwa na
Pan Africans, na baadaye alijiunga na vijana wa mitaa ya kishamapanda ya
mwanza Toto Africans na siku za hivi karibuni alikuwa na maafande wa
JKT Oljoro lakini sasa amebwaga manyanga kuwafua wanajeshi hao.
0 comments:
Post a Comment