Friday, April 12, 2013




Na Baraka Mpenja
Nyasi za dimba la kumbukumbu ya hayati Edward Moringe Sokonne jijini Mbeya zitahimili daluga za wanaume wa jeshi la magereza Wajelajela Tanzania Prisons dhidi ya wapigwa kwata wa Ruvu Shooting  kutoka maeneo ya Pwani ya Tanzania katika mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara utakaopigwa leo hii.
Prisons wataingia uwanjani wakiwa na hamasa kubwa baada ya kuwafumua Mgambo JKT kutoka Tanga “waja leo waondoka leo”  bao 1-0 jumatano ya wiki hii jijini humo.
Akizungumza na mtandao huu kutoka jijini Mbeya Kocha mkuu wa Prisons Jumanne Chale, amesema kikosi chake kipo shwari na wachezaji wake wamejengeka kisaikolojia kufuatia kupata ushindi adimu katika uwanja wao wa nyumbani.
“Kiukweli tunahangaika sana kutafuta ushindi katika uwanja wetu wa nyumbani, tangu tuingie katika ligi msimu huu tumeshinda mechi tatu tu nyumbani, hakika imetuumiza kwa siku nyingi, lakini ushindi dhidi ya Mgambo umetujengea imani ya kufanya vizuri leo hii”. Alisema Chale.
Chale ameongeza kuwa morali ya timu imekuwa kubwa baada ya wapenzi wa soka jijini humo kuamua kwa moyo mmoja kuwashangilia kufa na kupona ikiwa ni pamoja na kuwachangia fedha za kuwahamasisha.
“Sisi si yatima tena, kamati ya kutusaidia tushinde mechi zote zilizosalia chini ya kamanda wa Polisi mkoani hapa Diwani Athman Msuya imetupa nguvu sana na kama mambo yatakuwa hivi lazima tubaki ligi kuu”. Aliongeza Chale.
Kocha huyo ambaye aliwahi kuwanoa Africa Lyon kabla ya kusaini mkataba na Prisons alisisitiza kuwa hakika msimu huu umekuwa mgumu sana kwao kutokana na timu nyingi kuwa na wachezaji wazuri hivyo kusababisha ushindani mkubwa.
Wakati Prisons wakisema maandalizi yamekamili kwa ajili ya mchezo huo, nao Ruvu shooting waliopo mkoani humo, wamesema katika mchezo huo wenyeji wao hawatoki.
Kocha mkuu wa klabu hiyo, Charles Boniface Mkwasa  “Master” alisema wanajua mchezo huo ni muhimu sana kwao kutokana na ukweli kwamba kuna kamati maalumu iliyoundwa kuwasaidia Prisons wasishuke daraja, lakini bila shaka watachanga karata zao vizuri na kupata ushindi ugenini.
“Tumetoka kucheza na Polisi moro jumatano ya wiki hii, tulitoa suluhu nao, tumesafiri mpaka hapa mbeya, lengo letu ni kufuta matokeo mabaya tuliyoyapa hivi karibuni na kutafuta ushindi kwa nguvu zote”. Alijigamba Mkwasa.
Mtanange wa Tanzania Prisons dhidi ya Ruvu Shooting utakuwa wa kukata na shoka kutokana na wenyeji kuhitaji mzigo wa pointi tatu ili waendelee kujijengea mazingira salama ya kukwepa rungu la kuporomoka daraja, wakati Shooting wao wanahitaji nafasi nzuri zaidi katika msimamo wa ligi hiyo.
End…………………..

0 comments:

 
voyeur porn porn movies sex videos hd porno video