
Mabingwa wa soka Tanzania Bara na wawakilishi wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Yanga SC, leo wamefanikiwa kuwatungua wanajeshi wa APR ya Rwanda kwa mabao 2-1, mchezo uliopigwa kunako dimba la Amahoro nchini Rwanda.
Alikuwa ni Juma Abdul ambaye aliiandikia Yanga bao la kwanza dakika ya 21 baada ya kuachia mkwaju mkali wa adhabu ndogo na kutinga wavuni huku mlinda mlango wa APR akikosa la kufanya golini.
Wakicheza kwa kujiamini huku wakipiga pasi ndefu ndefu, Yanga walifanikiwa kuandika bao la pili kupitia kwa Mzimbabwe Thaban Kamusoko 'Scara' katika dakika ya 74 baada ya ya kugongeana kwa uzuri na Mzimbabwe mwenza Donald Dombo Ngoma.
APR walicharuka na kuanza kusaka walau goli la kufutia machozi na ndipo walipofanikiwa kuandika bao lao mnamo dakika ya 90 kupitia kwa Patrick Sibomana ambaye alitumia makosa ya kipa wa Yanga Ali Mustafa Mtinge alioutema mpira langoni mwake.
Yanga sasa wana hazina ya magoli mawili ugenini, hali ambayo inawarahishia kazi katika mchezo wa marudiano utakaopigwa baada ya wiki moja katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Takwimu muhimu.
- Yanga imekutana na APR FC kwa mara ya tatu kwenye michuano ya klabu bingwa barani Afrika. Mchezo wa kwanza kuzikutanisha timu hizo, Yanga ilikubali kichapo cha bao 1-0 lakini leo Yanga imeshinda kwa bao 2-1.
- Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite walikuwa wanacheza dhidi ya timu yao waliyowahi kuitumikia miaka kadhaa iliyopita.
- Kikosi cha APR kilichocheza dhidi ya Yanga kilikuwa na wachezaji wazawa kwa 100% wakati Yanga walikuwa na wachezaji mchanganyiko, wachezaji wazawa na wale wa kigeni.
0 comments:
Post a Comment