Mwisho wa juma hili kutapigwa michezo miwili kwenye jiji la Tanga, Jumamosi Yanga itakuwa ikiwakabili wenyeji Mgambo JKT wakati siku ya Jumapili itakutana miamba miwili ya soka ya mji wa Tanga African Sports dhidi ya Coastal Union kwenye uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Achana na mchezo kati ya Mgambo JKT dhidi ya Yanga, mchezo ambao ni habari ya mjini jijini Tanga ni ule wa siku ya Jumapili kati ya African Sports ‘wana-kimanumanu’ dhidi ya ‘wagosi wa Kaya’ Coastal Union. Mchezo huo umekuwa ni gumzo na umeteka wakazi wengi wapenda soka wa mji wa Tanga kutokana na kile kinachoaminiwa kuwa ni upinzani mkubwa uliopo kati ya timu hizi mbili.
Costal Union wakiwa wanatoka barababara ya 11 wakati African Sports wao wanatoka barabara ya 12 hizi ni timu ambazo ni majirani na kihistoria upinzani wao unatokana na namna ambavyo hizi timu zilivyoanzishwa na aina ya watu wambao walizianzisha.
African Sports ndiyo timu kongwe ukilinganisha na Coastal Union, yenyewe ilianzishwa mwaka 1947 na wazawa wa mji wa Tanga hapa unawazungumzia Wadigo, Wasambaa, na makabila mengine ambayo kiasili ni wazawa wa mji wa Tanga.
Baada ya Africans Sports kuanzishwa, kulikuwa na wakazi wengine wa mji wa Tanga ambao wao sio wazawa wa mji huo. Wengi wao walikuwa ni wale wenye asili ya Asia, wakawa wanatengwa na wazawa hasa linapokuja suala la kuishabikia timu ya African Sports kitu kilichopelekea na wao kuanzisha timu yao ambayo ni Costal Union.
Upinzani ukaendelea kuwa mkubwa kati ya wazawa dhidi ya wageni wa mji huo kupitia timu zao za African Sports na Coastal Union, hata timu hizi zilipokuwa zikikutana upinzani wao ulikuwa ukichagizwa na aina ya wachezaji waliokuwa wanacheza kwenye timu hizi. Wachezaji wengi ambao hawakuwa wazawa wa mji wa Tanga walikuwa wanacheza timu ya Coastal Union wakati wazawa walikuwa wanacheza kwenye timu ya African Sports.
Lakini hata hivyo bado ilikuwa ni nadra sana kuona wachezaji wanaotoka nje ya mji wa Tanga wanapata nafasi ya kucheza kwenye timu hizi mbili, Peter Tino ni moja ya wachezaji wachache waliopata nafasi ya kucheza kwenye timu ya African Sports akitokea nje ya mji wa Tanga. Kutokana na uwezo wake, akang’ara na kuwa kipenzi cha wakazi wa Tanga kama mzawa wa mji huo hiyo ilikuwa ni miaka ya mwanzoni mwa 1980.
Kwahiyo asilimia kubwa ya wachezaji wa African Sports pamoja na Coastal Union walikuwa ni wazawa wa mji wa Tanga. Hiyo ikawa inaleta upinzani kati ya mtoto wa nyumba ya kwanza dhidi ya mtoto wa nyumba ya pili na motto wa mtaa wa pili dhidi ya motto wa mtaa wa tatu. Lakini kadiri siku zinavyozidi kwenda mbele upinzani wa timu hizi umekuwa ukishuka.
Mara ya mwisho timu hizi zimekutana kwenye mchezo wa ligi kuu ilikuwa ni mwaka 1991 mchezo uliomalizika kwa sare ya kufungana goli 1-1 na mwaka uliofuta African Sports ikashuka daraja na hawakupanda tena hadi mwaka huu walipoweza kurejea tena kwenye ligi kuu ya soka Tanzania bara.
Jumapili wanakutana kwenye mchezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara wakiwa kwenye mazinira tofauti, upinzani wa timu hizi sio kama ule wa miaka ya nyuma na sababu kubwa ya kushuka kwa upinzani huu ni kupungua kwa wachezaji wazawa katika vilabu hivi. Kikosi cha sasahivi cha African Sports kina wazawa wasiozidi 12 huku kikiwa na wachezaji zaidi ya 10 wanaotoka nje ya Tanga wakati kikosi cha Coastal Union kinawachezaji nane ambao ni wazawa wa Tanga huku kikiwa na wachezaji 15 kutoka nje ya mkoa wa Tanga.
Coastal Union ipo nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi kuu ikiwa imecheza michezo 10 imeshinda mchezo mmoja imetoka sare michezo minne na kufungwa kwenye michezo mitano, inaponti saba zinazoifanya ikae nafasi ya 13.
African Sports wao wako nafasi ya mwisho (16) wakiwa na jumla ya pointi tano baada ya kucheza michezo tisa nakufanikiwa kupata ushini kwenye mchezo mmoja wakipoteza michezo mingine hadi sasa kwenye ligi hiyo ambayo itaendelea tena Jumamosi December 12.
0 comments:
Post a Comment