Wachezaji wa Yanga ambao timu yao inashika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara. Ligi hiyo itasimama kuanzia leo.
MABOSI wa Yanga wameonekana kuridhika na mwenendo wa kikosi chao katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara, lakini Mkuu wa Benchi la Ufundi la klabu hiyo, Kocha Hans Pluijm, ameshusha mkwara mzito kwa wachezaji wake akiwaambia atakayezingua ajiandae kuzinguliwa.
Pluijm amesema mchezaji yeyote ambaye atashindwa kufanya vema katika kikosi chake, asitarajie mbeleko ya kumbeba na kuwasisitiza kila mmoja kujipanga kisawasawa na kutumia vema nafasi wanazopewa uwanjani.
Akizungumza na Mwanaspoti, aliongeza kuwa kamwe hawezi kuzungumzia mapungufu ya wachezaji wake hadharani na jambo hilo atalifanya katika vikao vyake vya ndani, lakini hatakuwa na uvumilivu kwa mchezaji yoyote atakayeleta masihara katika mechi zao.
Pluijm ambaye sasa anakuna kichwa kujiuliza awape mapumziko ya muda gani wachezaji wake, alisema anataka kuona kila mchezaji akijituma kwa kiwango kikubwa ambapo kwa yoyote atakayeonekana kutokuwa tayari kuitetea klabu, hatakuwa na nafasi katika kikosi chake.
Amesema kwa sasa kila mchezaji aliyepo katika kikosi hicho ana nafasi ya kuitumikia timu hiyo ambapo muhimu ni juhudi zake kuhakikisha mabingwa hao wanaibuka kidedea katika mechi zao.
“Ukiwa kocha busara muhimu ni kujua maeneo ya muhimu ya kuwakosoa wachezaji wako juu ya mapungufu yao, lakini kwa sasa hakuna mjadala wa kuvumilia mchezaji anayeonekana kutokuwa tayari kuitetea Yanga,” alisema Pluijm.
“Nataka kuwa na wachezaji wenye kiu ya mafanikio, tuna kikosi kipana chenye wachezaji wanaoweza kupambana kitu pekee kitakachompatia mchezaji husika nafasi ni ubora wake na umakini ulio sawasawa katika mechi zetu.” Yanga ilikuwa ugenini Kanda ya Ziwa ambapo ilipata sare ya mabao 2-2 kwa Mwadui Shinyanga kabla ya kuizabua Kagera Sugar kwa mabao 2-0 juzi Jumamosi na kufikisha pointi 23.
Chanzo:Mwanaspoti
0 comments:
Post a Comment