Hii ni njia inayotumika kutambua mpira uliovuka
mstari wa goli katikati ya nguzo mbili zilizosimama na ile nguzo inayounganisha
nguzo mbili zilizosimama (mtambaa wa panya) pamoja na mstari uliochorwa chini
ya mtambaa wa panya pia vifaa vya umeme/ kielekroniki (electronic devives)
hutumika katika kumsaidia refa kuzawadia goli au la.
Lengo la teknolojia ya goli si kuondoa kazi za waamuzi bali kuwasaidia katika
kufanya maamuzi. Teknolojia ya goli ni lazima ioneshe wazi kama mpira wote
umevuka mstari na hii taarifa itatumika kumsaidia refa katika kufanya maamuzi
yake ya mwisho. Baada ya malumbano na mijadala mbalimbali kuibuka katika ligi
kuu ya Uingereza, Kombe la Dunia – 2010, na Kombe la Mataifa ya Ulaya – 2012,
FIFA (ambayo mwanzoni ilikuwa ikiipinga teknolojia hii) iliamua kupima
teknolojia tisa lakini ni mbili tu zilizokubalika.
Tarehe 5 Julai 2012, Bodi ya Kimataifa ya Mpira wa
Miguu (IFAB – International Football Association Board) iliruhusu matumizi ya
teknolojia ya goli, na kubadilisha sheria za mchezo kuruhusu (lakini si
kulazimisha) matumizi.
Ni mifumo (Systems) miwili tu ndio ilipitishwa
kutumika, wa kwanza ukiwa ni Goli la Refa (GoalRef) na wa pili ukiwa ni wa
Jicho la Mwewe (Hawk-Eye). Desemba 2012, FIFA ilitangaza kuitumia teknolojia ya
goli katika mechi za mashindano kwa mara ya kwanza katika Kombe la Dunia –
2014. Kuanzia mwaka 2013, teknolojia hii ilianza kutumika katika ligi kuu ya
soka nchini Marekani lakini timu za Canada zinazoshiriki ligi hiyo hazitumii
teknolojia hii zinapocheza nyumbani kutoka na ukosefu wa fedha.
Teknolojia ya goli iliwekwa katika viwanja vyote 12
vilivyotumika katika Kombe la Dunia – 2014 nchini Brazili. Teknolojia hii sasa
inatumika katika ligi maarufu zaidi kwa kandanda duniani, Ligi Kuu ya
Uingereza.
Sheria
Tangu 2012, sheria hii imeruhusiwa kutumika kwenye
mechi. Lakini pia si lazima kuitumia, gharama yake na upya wake katika jamii ya
wanasoka inamaanisha inaweza kutumika katika mechi za mashindano makubwa tu.
Haya ni baadhi ya maneno yanayoweza kupatikana
katika sheria za mchezo yakihusu teknolojia hii:
·
Sheria namba 1 (Uwanja wa mchezo):
inaruhusiwa kufanya maboresho katika fremu ya goli.
·
Sheria namba 2 (Mpira): inaruhusiwa
kutumia mpira ulio na teknolojia hiyo ndani yake.
·
Sheria namba 5 (Refa): inamtaka refa
kupima kama teknolojia ya goli inafanya kazi kabla ya mechi na endapo atagundua
mapungufu yeyote basi asiitumie.
·
Sheria namba 10 (Njia ya Ufungaji Goli) :
Kuruhusu matumizi ya teknolojia ya goli ili kujua kama goli limefungwa au la. Inasema,
“Matumizi ya teknolojia ya goli lazima yaoneshwe kwenye sheria za mashindano
husika”
Ukosoaji
Mawakili wa teknolojia ya goli wanaendelea kusema
kuwa itapunguza makosa ya refa kwa sehemu wakati wa mchezo lakini bado kuna ukosoaji
wa teknolojia hii umeendelea kuwepo. Ukosoaji mwingi umetokea ndani ya FIFA
wenyewe pamoja na Rais wa FIFA, Sepp Blatter. Pamoja na kuwepo ukosoaji katika
teknolojia mbili zilizopitishwa, wakosoaji wanasema itaondoa ile hali ya
kibinadamu ndani ya mchezo na pia
itapunguza ladha ya majadiliano
yanayotokana na makosa yaliyofanyika katika mchezo husika. Sepp Blatter amewahi
kunukuliwa akisema, “Michezo mingine imekuwa ikibadilisha sheria zake ili
kuendana na teknolojia mpya..... Sisi
hatufanyi hivyo na hii inafanya mpira wa miguu uvutie sana na kuwa maarufu
zaidi”
Wakosoaji wengine wanasema itakuwa ni gharama sana
kuiweka teknolojia hii katika kila daraja la mchezo hasahasa katika vyama
vidogo vya mpira na maskini. Watu wenye sauti FIFA wameelezea kupendezwa zaidi na
dhana ya ‘Ubora wa maamuzi’ kwa kuongeza idadi ya marefa na sio kuitumia
teknolojia hiyo.
Blatter yeye alikuwa akiipinga teknolojia hii hadi
pale goli la Frank Lampard wa Uingereza
lilipokataliwa katika Kombe la Dunia – 2010 ambapo mpira ulionekana wazi kuvuka
mstari wa goli.
Utambulisho wa marefa watano yaani marefa wengine wawili
kusimama nyuma ya goli kila goli moja refa mmoja, ilikuwa ni sehemu ya kusaidia
matukio kama haya.
Gharama
Mwanzoni wa mwaka 2014, timu nyingi zinazoshiriki
ligi kuu ya soka ya Ujerumani – Bundesliga walipiga kura ya hapana kukataa
teknolojia hii ya goli kutokana na sababu za kifedha. Kila klabu moja
ingetakiwa kutoa € 250,000 (zaidi ya milioni mia tano, shilingi za Tanzania)
kwa ajili ya kuweka kadi ndani ya mpira hadi € 500,000 (zaidi ya bilioni moja,
shilingi za Tanzania) kwa ajili ya teknolojia ya Jicho la Mwewe. Kocha wa klabu
ya 1. FC Cologne, Jorg Schmadtke, alitoa majumuisho ya kura kwa kusema, “Gharama ni kubwa sana na hii
(teknolojia) haikubaliki”
Ilitazamiwa FIFA ingepata Paundi 300,000 kutokana na
ligi kuu ya Uingereza kuamua kuitumia teknolojia hii. Kila klabu ilitoa Paundi
15,000 kwa ajili ya kuweka, kuipima na kupata nembo ya ubora wa FIFA kwa kamera
za Jicho la Mwewe. Pia FIFA ilipata paundi zingine 15,000 kwa ajili ya Uwanja
wa Wembley ambao hutumika katika mechi za nusu fainali na fainali za Kombe la
FA pamoja na fainali ya Kombe la Ligi.

.jpg)
0 comments:
Post a Comment