Wednesday, May 20, 2015

Niliufuatilia kwa umakini mkubwa mchezo wa marudiano wa nusu fainali ya klabu bingwa barani Ulaya baina ya klabu ya Real Madrid waliokuwa wenyeji wa Kibibi kizee cha Turin, klabu ya Juventus ya nchini Italia.
Kabla ya mtanange ule ni watu wachache mno ambao waliipa nafasi Juventus. Pengine utetezi wa kombe hilo kwa klabu ya Real Madrid uliwafanya mashabiki wengi waamue kuipa matokeo klabu hiyo yenye jina kubwa katika mawanda ya soka ya kimataifa.
Kabla ya mchezo wa kwanza kuna mengi ambayo yaliandikwa kuhusu mchezo huo huku Madrid wakionekana kupewa nafasi kubwa zaidi kuliko Juventus. Hapana shaka uwepo wa wachezaji ghali zaidi katika timu hiyo ilikuwa sababu ya watu kuamini hivyo japo siku zote mpira hauchezwi nje ya uwanja, bali huchezwa ndani ya uwanja tena hadharani.
Binafsi niliufuatilia kwa jicho la tatu mchezo wa marudiano ambapo pamoja na akina Cristiano Ronaldo, Karim Benzema, Gareth Bale na James Rodriguez kupambana lakini hawakufua dafu mbele ya jeshi la Maxmilliano Allegri. Akina Alvaro Morata, Paul Pogba, Carlos Tevez na Patrice Evra walizuia mianya yote ya wachezaji hao kuutawala mchezo huo.
Ni katika mchezo huo, safari adhimu ya klabu kubwa na tajiri ya Real Madrid katika mbio za kuutetea ubingwa wake wa Klabu bingwa barani Ulaya (UEFA) ziligonga mwamba na kuwafanya mashabiki wake kote duniani kubaki babaikoni.
Vijana wa Maximilliano Allegri waliingia uwanjani kwa lengo moja tu, kupata matokeo chanya na hata kucheza fainali ya UEFA msimu huu. Ndivyo ilivyokuwa, mwisho wa siku Alvaro Morata hakufanya ajizi, akicheza katika uwanja aliouzoea pengine kuliko viwanja vyote duniani haikumuwia vigumu kufanya yake pale Santiago Bernabeu.
Ulikuwa ni usiku wa heri kwa wachezaji wa Juventus, usiku wa shangwe kwa Mashabiki wa mchezo wa soka wa nchini Italia, usiku wa raha mustarehe kwa kocha Allegri. Akina Patrice Evra, Carlos Teves, Morata na Paul Pogba walikuwa wanaupambanua ukulu wao katika mawanda ya usakataji wa kabumbu na hata kuwaacha mashabiki wa Real Madrid wakibaki na labda.
Kila nilipomtazama Morata nilijikuta nikishawishika kumfuatilia hatua kwa hatua. Uchezaji wake ulikuwa hauchoshi kama akina Ronaldo ambao mpaka mechi inamalizika nilishindwa kujua namba aliyokuwa anacheza kwa siku ile.
Hapana shaka Mhispania huyu aliyezaliwa miaka 23 iliyopita jijini Madrid pale Hispania alitaka kumwonesha bosi wake wa zamani Carlo Ancelotti kuwa alifanya makosa makubwa kumuachia kizembe.
Ni wazi kuwa Morata pamoja na akina Evra, Pogba, na Carlos Tevez ni mfano wa jiwe la msingi ambalo kabla yake lilikataliwa na waashi ambapo mwisho wa siku likaja kuwa jiwe kuu la pembeni.
Morata aliyewahi kubezwa pale Madrid amekuwa Lulu pale Turin. Paul Pogba ambaye aliondoka akiwa huru pale Manchester United, kwa sasa saini yake inasakwa kwa udi na uvumba na vilabu vingi tajiri duniani ikiwepo Manchester yenyewe.
Patrice Evra ambaye aliondoka Manchester United eti kwa sababu alikuwa ameshuka kiwango hakutoa mwanya kwa washambuliaji wa Madrid kuleta madhara langoni kwake. Kama ilivyo kwa Carlos Tevez ambaye alionekana kuwasumbua sana walinzi wa Madrid.
Ulikuwa ni mchezo ambao pengine Mwenyezi Mungu alikuwa na makusudi yake. Makusudi ya kuupambanua upeo wa binadamu kuhusu maamuzi anayoyafanya kabla. Tamati ya michezo yote miwili ilitoa jibu la maswali mengi kwa wanafamilia wengi wa mchezo wa soka ulimwenguni.
Pamoja na kufunga goli la kwanza katika mchezo wa awali uliopigwa pale Turin siku kadhaa zilizopita, hakuwa na sababu ya kushindwa kufanya hivyo tena pale Santiago Bernabeu, kwa dhati ya moyo wake aliisawazishia timu yake goli ambalo moja kwa moja liliipeleka Juventus katika fainali.
Akina Benzema, Rodriguez, Bale na Ronaldo walionekana kutokuwa katika ubora wao. Pengine umuhimu wa mchezo ule uliwafanya wacheze tofauti kutokana na akili yao kuwaza kitu kimoja tu, Ushindi! Ndoto ambayo ilionekana kuzimwa kabisa na wachezaji wa Juventus huku nikimshuhudia mchezaji ghali zaidi duniani Gareth Bale akipiga mashuti mengi nje ya lango (Off target shoots).
Kwa upande wangu mlinda mlango Iker Cassilas ndiye alionekana kucheza kwa kiwango cha hali ya juu na hata kuwazidi wachezaji wa ndani wa timu yake, huku beki namba tatu Marcelo akionekana kuibeba Madrid katika mchezo ule tofauti na wachezaji wengine ambao kwayo nilitegemea wangefanya makubwa katika mtanange ule lakini ikawa tofauti.
Acha tu nirejelee aya hii ya Biblia “Jiwe walilolikataa waashi, limekuwa Jiwe Kuu la pembeni” (Mk. 12:10). Kuna mengi sana ya kuandika kuhusu mchezo wa soka hususan nusu fainali ile. Lakini kwa leo acha tu niishie hapa, hapana shaka somo langu kuhusu ubora wa akina Morata dimbani limeeleweka.
Ngoja tuisubiri tarehe 6 Juni, tuweze kumpata bingwa stahiki wa michuano hii baada ya bingwa mtetezi kuondoshwa mashindanoni.
*Imeandikwa na Oswald Ngonyani, mwandishi/mchambuzi wa michezo wa Gazeti la Dimba, kwa wenye Maoini/Ushauri wanaweza kutuma kwenda namba 0767 57 3287.
CHANZO: DIMBA Jumapili Mei 17, 2015

0 comments:

 
voyeur porn porn movies sex videos hd porno video