WAPENDA soka na watanzania wote kwa ujumla wamejawa na majonzi baada ya jana wanachama 7 wa Tawi la Mpira na Maendeleo la klabu ya Simba maarufu kama Simba Ukawa kufariki duniani katika ajali ya gari lao aina ya Toyota Costa Mkoani Morogoro walipokuwa wakisafiri kwenda Shinyanga kuipa nguvu timu yao katika mechi ya leo ya ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar inayopigwa uwanja wa CCM Kambarage.
Taarifa hizi zilishitua wengi kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii na vyombo vingine vya habari. Hakika ziliwagusa wengi na kuwaacha wakiwa na majonzi makubwa.
Mtandao huu ulipokea taarifa hizi na kuanza kufuatilia na kuwafahamisha Watanzania kinachoendelea na mpaka kufika jana saa mbili usiku, watu hao 7 walithibitishwa kufariki na vyombo vya usalama mkoani Morogoro.
Kutokana na majonzi haya, mtandao huu unatuma salamu za Pole kwa klabu ya Simba kwa kuondokewa na watu hawa muhimu.
Licha ya kuwepo kwa tofauti zao na mitazamo, lakini bado kibinadamu lazima wameumizwa na msiba huu mzito.
Kwa muda mrefu Simba Ukawa wamekuwa na mgogoro na viongozi wa Simba uliotokana na kutofautiana mawazo, lakini kupata ajali ni jambo jingine.
Mwenyezi mungu awape moyo wa subiri na kuwatia wapesi wanasimba wote, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu wote.
Masikini hawakujua nini kitatokea, wangejua wasingesafiri, lakini siku zote kazi ya Mola haina makosa. Wapumzike kwa amani mahala pema peponi.
Tunasikitishwa na tunaendelea kusikitishwa na baadhi ya watu wachache wanaofurahia tukio hili baya la ajali na watu kupoteza maisha.
Mitandao ya kijamii ina uhuru wake, mtu huandika anachotaka na kwa bahati mbaya hakuna sheria.
Baadhi ya watu wasiokuwa waungwana walifurahia kufariki kwa baadhi ya wanachama wa Simba Ukawa kwa madai kuwa wanawasumbua Simba.
Kugongana kimawazo jambo la kawaida, lakini matatizo yanapotokea hakuna uhasama tena. Hivi wewe unayecheka yaliyowakuta Ukawa, unajua dakika 2 zijazo nini kitatokea kwako?
Kifo hakina mzaha ndugu yangu, kila nafsi itaonja mauti. Tonafautiana siku tu, wakati wako utafika na utapumzika hata kama si kwa ajali kama Simba ukawa.
Tumechukizwa sana na watu wanaochekelea, hakika Mungu awasamehe.
Poleni sana Simba, poleni sana Watanzania wenzangu!



0 comments:
Post a Comment