Na Ezekiel Kamwaga
Wakati nilipokuwa Msemaji na hatimaye Katibu Mkuu wa Klabu ya
Simba, hakuna tawi nililokuwanalo karibu kama lile la Mpira na Maendeleo. Kulikuwa na sababu kuu mbili, mosi ilikuwa ni
ukaribu wake na ofisi yangu na pili ubunifu iliokuwa nao.
Ukaribu ninaouzungumzia ni ule kwamba mara nyingi walikuwa
wakifanya shughuli zao katika eneo la Makao Makuu ya Klabu ya Msimbazi jijini
Dar es Salaam. Haikuwa rahisi kupita siku moja ya kazi pasipo kukutana na walau
mwanachama mmoja wa tawi hilo.
Ubunifu ninaouzungumzia ni ule wa tawi lile kutengeneza vitu
kama kalenda na picha ambazo baadaye waliziuza na kupata fedha za kuendeshea
shughuli zao.
Ni katika mazingira hayo ya kazi, ndipo nikakutana na mtu
aliyeitwa Mohamed Kingolile maarufu kwa jina la utani la ‘Ngumi Jiwe’ aliyefariki dunia katika ajali ya basi wiki iliyopita
mjini Morogoro wakati yeye na wenzake wakiwa njia kwenda mkoani Shinyanga
kutazama mechi baina ya Simba na Kagera Sugar. Wanachama sita walifariki katika
jail hiyo.
Yeye ndiye aliyekuwa Katibu wa Tawi na kwa namna zaidi ya
moja; kiongozi wa tawi hilo.
Viongozi wengi wa Simba, na vilabu vingine hapa nchini,
katika ngazi ya matawi wamefariki dunia na sikuwahi kuwaandikia tanzia. Leo,
nimewiwa kumuandikia Ngumi Jiwe kwa
sababu ya kuwaenzi watu wote wa aina yake waliotangulia mbele ya haki bila
kufahamika kitaifa ingawa walikuwa na mchango mkubwa kwenye mchezo wa soka.
Kingolile na wenzake katika kundi hilo, walikuwa
wakihakikisha wamefika klabuni kuanzia saa 12 na nusu asubuhi hadi saa mbili
asubuhi kwa ajili ya kupiga soga za mchezo wa soka.
Mijadala hii ilikuwa muhimu kwa watu ambao hawakwenda
kutazama mechi iliyopita ya Simba au hawana kuelewa kuhusu habari mpya
inayoihusu klabu. Kwa wafanyakazi wa mjini ambao wanalazimika kufika mjini
kabla ofisi zao hazijafunguliwa, Msimbazi ni ‘kijiwe’ cha kupotezea muda kabla
watu hawajaenda kwenye shughuli zao.
Watu wengi hawafahamu lakini kwenye kundi la Mpira na Maendeleo kuna mtu pale anaitwa
Chinga kutokana na kwamba anatoka mikoa ya Kusini mwa Tanzania lakini wenzake
wanamwita Shafih Dauda. Amepewa jina hilo kwa sababu ya uwezo wake wa kuelezea
mchezo.
Yaani, kuna watu wanampa fedha ili aende kuangalia mechi
uwanjani ili baada ya mchezo, iwe kesho yake au siku yoyote, aweze kuwaeleza
wasiokwenda kuhusu kilichotokea. Kama kuna mchezaji mpya kasajiliwa na Simba na
amefanya mazoezi kwa siku moja tu na Chinga akamuona, muulize tu na atakwamba
kama mchezaji ni mzuri au mbaya.
Akina Ngumi Jiwe pasipo
kuwa na uwezo wa kifedha, walikuwa tayari kusafiri kwa gharama yoyote kwenda
popote ambako Simba inacheza. Mara nyingi wakiwasili katika mkoa husika siku
ileile ya mechi na kugeuza kurudi Dar es Salaam mara baada ya mechi.
Ngumi Jiwe ni
miongoni mwa watu waliokuwa tayari kufanya lolote kuisaidia Simba ipate
ushindi. Kuna mambo mengi ya kuitafutia klabu ushindi alikuwa akiyafanya ambayo
kwa sababu maalumu sitayataja katika makala hii.
Mara nyingi Kingolile alikuwa anakaa katika kiti cha mbele
upande wa pili wa dereva wakati wanaposafiri. Lengo lilikuwa ni kuweza kusikika
kwa urahisi wakati anapotaka kutoa taarifa akiwa ndani ya gari lakini pia akiwa
pale mbele watu wanaoliona basi wanajua Ngumi
Jiwe yupo.
Katika mpira wa Tanzania ambao bado haujafanyiwa mikakati
mikubwa ya kutangazwa, mabasi ya washabiki ni sehemu moja ya hamasa
zinazotangaza mchezo huu. Hata kama mtu alikuwa hana mpango wa kwenda mpirani,
yale mashamsham ya kina Kingolile barabarani huwafanya watu kubadili mawazo na
kuja viwanjani.
Siku zote ninaamini kuwa watu kama akina Kingolile ndiyo
wanaofanya washabiki wa mpira waendelee kwenda viwanjani hapa nchini wakati
katika nchi jirani idadi inapungua kila kukicha.
Niliwahi kwenda kutazama mechi ya Ligi Kuu ya Soka ya Uganda miaka
miwili iliyopita katika Uwanja wa Mandela jijini Kampala, na nilisikitika kuona
watu chini ya 400 wakiwa wamekwenda kutazama mechi hiyo.
Ukichunguza kwa makini, pamoja na sababu nyingine zinazotajwa
ikiwamo nguvu ya Ligi Kuu ya England, utabaini kuwa mojawapo ya sababu ni nchi
hiyo kutokuwa tena na akina Kingolile na matawi ya vilabu kama Mpira na Maendeleo, Mpira Pesa, Wekundu wa Terminal, Yanga Bomba na mengine.
Watu wanaofanya mchezo huu uzidi kuvutia, kama akina
Kingolile, yule Yamungu wa Morogoro na wengineo, wanapaswa nao kutambulika kama
sehemu ya watu wanaopaswa kuheshimiwa. Hawa ni watu ambao maisha yao yote
wameyatoa kwa sababu ya mchezo huu.
Sikumbuki kama nimewahi kuzungumza na Ngumi Jiwe kuhusu jambo lingine lolote zaidi ya mchezo wa soka na
klabu ya Simba. Leo atakuja na hili na kesho atakuja na lile. Lakini kila siku
yeye ni Simba tu na si kingine.
Kwa bahati mbaya sana, watu wa namna hii, kwa sababu
hawakuwahi kushika nyadhifa za juu kwenye vilabu hivi vikubwa, wanapokufa
huondoka na mambo yao. Kinachouma ni kwamba, watu huwa hatupotezi muda wetu
kuwaelewa.
Mimi ni mmoja wa watu waliosikitika baada ya kusikia
Kingolile na wenzake wamepigwa mkoani Morogoro baada ya mechi dhidi ya Polisi eti
kwa madai ya kuihujumu Simba. Ngumi Jiwe
ninayemfahamu mimi asingeweza kuihujumu Simba. Ataihujumu vipi timu ambayo
ikifungwa anapata maradhi?
Angeweza vipi kuihujumu timu ambayo alikuwa akipiga ngoma na
kucheza kwa dakika zote tisini wakati ikicheza pasipo kujali imefungwa au la?
Angewezaje kuihujumu timu ambayo sasa amemwaga damu yake kwayo?
Kama kuna jambo ambalo wana Simba wanatakiwa kulifanya sasa
ni kuondoa ile dhana kwamba kuna wanachama ambao hawaitakii mema klabu. Damu
hii ya wanachama sita waliokufa kwenye ajali na wengine waliojeruhiwa inatakiwa
imwagilie mti wa amani na maelewano.
Mtawala wa zamani wa Ulaya, Attila, alipata kusema miaka
mingi iliyopita kwamba “ Si kila mpinzani wako ni adui”. Inawezekana kuna aina
fulani ya upinzani ndani ya klabu lakini hali hii haiwezi kufanywa kuwa uadui
wa wanachama kupigana wenyewe kwa wenyewe.
Chukulia tu kwamba kwenye nchi yetu kuna CCM, CUF, Chadema na
vyama vingine ambavyo japo vinakinzana lakini wanachama wake wanazungumza na
kucheka pamoja. Inawezekana pia ndani ya Simba kukawa na Ukawa, Mpira Pesa na
makundi mengine.
Kuna tofauti za kisera na kimtazamo kuhusu mambo fulani
lakini Umoja unatakiwa ubaki palepale. Kama anayetakiwa na Simba Ukawa akiwa madarakani isiwe nongwa na anayetakiwa na Mpira Pesa akishinda isiwe nongwa pia
kwani wote wanajenga nyumba moja.
Kama ningekuwa kiongozi wa Mpira na Maendeleo leo ningeagiza kwamba itengenezwe bendera kubwa
yenye rangi nyekundu na nyeupe ambayo ina picha ya Kingolile itakayokuwa
uwanjani kila Simba inapocheza. Hata kama kimwili hayuko nasi, atakuwepo uwanjani
kiroho kila wakati klabu inapocheza !
Kama ambavyo Bill Shankly, Bob Paisley na Joe Fagan
wanavyoonekana kwenye Uwanja wa Anfield kila Liverpool inapocheza. Ni kwa namna
hii pekee ya kuwaenzi watu kama Ngumi
Jiwe, ndivyo ambavyo tutawatengeneza wengi wengine. Na soka letu litazidi
kupata washabiki.
Ingawa Kingolile ameondoka, ni imani yangu kwamba kile
alichofanya kitaendelea kufanywa na wengine wa aina yake. Watu kama Fihi Kambi,
Ustaadh Masoud, Abdallah Kazumari, Chinga, Martin Kumalija, Haruna Nazi, Makoye
na wengine ambao maisha yao wameyatoa kwa ajili ya klabu ya Simba na mpira wa
Tanzania kwa ujumla wake.
Kwa namna yao waliyoamua.
Mungu awalaze pema peponi marehemu wote waliofariki katika
ajali ya Morogoro ya basi la Mpira na
Maendeleo.
Mwisho


0 comments:
Post a Comment