.jpg)
Na Bertha Lumala, Dar es Salam
Kesi ya madai ya fidia inayomkabili kipa mkongwe Juma Kaseja dhidi ya Yanga SC imeshindwa kusikilizwa leo jijini hapa kutokana na nyaraka za kesi hiyo kuungua.
Kesi hiyo imefunguliwa na Yanga SC kwenye Tume Usuluhishi na Uamuzi wakitaka kipa huyo wa zamani wa Simba SC awalipe mamilioni ya shilingi kutokana na kuvuna mkataba.
Hata hivyo, Tume hiyo imeshindwa kusikiliza shauri hilo la madai ya fidia, ada ya usajili na kuvunja mkataba vyenye thamani ya jumla Sh. milioni 340 dhidi ya Kaseja, baada ya nyaraka za shauri hilo kuteketea kwa moto katika ofisi ya wakili wake, Samson Mbamba.
Shauri hilo lilikuwa limepangwa kusikilizwa usuluhishi leo mbele ya Msuluhishi Alfred Masse.
Hata hivyo, wakili wa utetezi, Mbamba ameomba muda kutokana na nyaraka zote kuhusu madai hayo kuteketea kwa moto ndani ya ofisi yake ya masuala ya uwaliki na sheria.
Mbamba ameomba upande wa mlalamikaji umpatie nakala nyingine kupitia wakili wa Yanga SC, Frank Chacha ili aweze kuendelea na usikilizwaji na shauri hilo la aina yake kisoka mwaka huu.
Tume imekubali maombi hayo na shauri hilo litasikilizwa Machi 11.
Novemba 11, mwaka jana Kaseja alitoa hati ya kusitisha mkataba wa kuichezea Yanga SC kupitia wakili Mbamba kwenda kwa klabu hiyo ya Jangwani.
Aidha, Januari 20, mwaka huu Yanga SC, mabingwa mara 24 wa Tanzania Bara, walifungua kesi dhidi ya Kaseja wakimdai fidia pamoja na mambo mengine kedekede huku wakitaka awalipe Sh. milioni 340 za Kitanzania.
0 comments:
Post a Comment