Kocha mkuu wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime (wa kwanza kulia) akiwa kazini
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MTIBWA Sugar wamepania kufanya vizuri na kurejesha
makali yao ya nyuma katika michuano ya ligi kuu soka Tanzania bara inayotarajia
kuanza septemba 20 mwaka huu.
Wakata miwa hao wa Manungu, Turiani, mkoani
Morogoro, wataanza kampeni za kusaka ubingwa dhidi ya Yanga, septemba 20 mwaka
huu katika uwanja wa nyumbani wa Jamhuri mkoani Morogoro.
Kocha mkuu wa mabingwa hao wa Tanzania kwa mwaka
1999 na 2000, Mecky Mexime ameiambia MPENJA BLOG kuwa licha ya kubomolewa kwa
kikosi chake, maandalizi yanakwenda vizuri na vijana wapya waliopatikana katika
usajili wa majira ya kiangazi wanazidi kuimarika .
Mexime amekiri kuwa kila mwaka anakuwa na kazi
ngumu ya kuijenga timu upya kwasababu wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza huwa
wananunuliwa na timu nyingine zikiwemo Simb na Yanga,hivyo anashindwa kuonesha
kiwango cha juu.
Katika kikosi cha Simba wachezaji wakubwa kama
Shaaban Kisiga, Awadh Juma na Hussein Sharrif wametokea Mtibwa siku za
karibuni, ingawa Awadh alisajili msimu uliopita.
Hussein Javu wa Yanga naye alisajiliwa kutoka
Mtibwa Sugar msimu uliopita.
“Kwanza tunamshukuru Mungu kwasababu tunaendelea
vizuri. Tatizo ni kwamba kila mwaka ninajenga timu upya. Lakini kinachotusaidia
ni kwamba Tanzania tuna vipaji vingi na tumechukua vipaji vipya na timu
inaendelea vizuri.” Alisema Mexime.
“Kwa muda mrefu Mtibwa haijafanya vizuri na tatizo
ni ndio hilo kwamba kila mwaka tunajenga timu, lakini tunajiandaa vizuri licha
ya kuwepo matatizo mbalimbali”.
“Kikubwa unapoijenga timu upya unaangalia kwanza
nyuma, jinsi ya kujilinda na hatimaye jinsi ya kushambulia. Kwasasa timu
inalinda na kushambulia vizuri kwa kutengeneza nafasi, lakini tatizo linabaki
kufunga”.
“Ni tatizo tunalopambana nalo na naamini kabla ya ligi
kuanza tutakuwa sawasawa. Niwaambie mashabiki wa mpira wa Mtibwa Sugar na wa
Tanzania kwa ujumla watuombee kila la heri”.

0 comments:
Post a Comment