
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Tel:
0712461976
ZIMEBAKI saa chache kuwapokea washambuliaji wawili
wa Tanzania wanaocheza soka la kulipwa katika klabu ya TP Mazembe ya nchini demokrasia
ya Congo, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu.
Kuwasili kwa nyota hawa wawili kumefufua matumaini
kwa benchi la ufundi na jana kocha mkuu Mart Nooij alisema kuongezeka kwa
Samatta na Ulimwengu kumekifanya kikosi chache kiwe na nguvu zaidi katika safu
ya ushambuliaji.
Wanandinga hao wa Tanzania jana waliichezea TP
Mazembe katika mechi ya kwanza ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi
ya El Hilal Omdurani ya Sudan na kupigwa bao 1-0 ugenini.
Licha ya uchovu wa mchezo huo na safari
waliyoianza leo asubuhi, haitawazuia kuitumikia timu yao ya taifa ya Tanzania,
Taifa stars katika mchezo muhimu wa kesho dhidi ya Zimbabwe.
Taifa stars inahitaji kufunga magoli mengi katika
mchezo wa kesho ili kujiweka mazingira mazuri ya kusonga mbele.
Kwa muda mrefu sasa Stars imekuwa ikivurunda,
lakini kuja kwa kocha mpya kunawafanya watanzania wawe na hamu ya kufuatilia nini
kitatokea.
Nooij ameiongoza Stars katika mechi moja tu dhidi
ya Malawi kwenye uwanja wa sokoine jijini Mbeya na kutoka suluhu ya bila
kufungana, lakini mechi ya kesho ni ya kwanza ya kimashindano kuiongoza timu ya
taifa ya Tanzania.
Kila mtu ana hamu kuona mfumo wake wa uchezaji na
jinsi atakavyowatumia wachezaji wa Stars ambao jana aliwasifu kuwa na vipaji
vikubwa na uzoefu katika mashindano ya kimataifa.
Nooij alisema katika mchezo huo hawatacheza kwa
kushindana mithiri ya vita dhidi ya Zimbabwe, bali wataingia na kucheza mpira
kama walivyojiandaa.
Ili Taifa stars ifanye vizuri kesho, kuna baadhi
ya mambo yanatakiwa kuzingatiwa na wachezaji. Najua wamefundishwa, lakini
kilichobaki ni kuyatekeleza kwa nidhamu ya kimpira.
![]() |
Samatta na Ulimwengu wanatua Dar leo mchana |
Mosi; Wachezaji wetu watatakiwa kuwa shupavu,
kucheza kwa kasi, kuzuia kufungwa, na kucheza kwa weledi mkubwa kwasababu
nidhamu ya kimchezo ya wapinzani wao ni kubwa na wana watu wanaoweza kuamua
matokeo wakati wowote akiwemo mshambuliaji hatari, Knowledge Musoma.
Pili; kila mchezaji wa Taifa stars atatakiwa
kutimiza wajibu wa kazi yake kwa kuzingatia nafasi aliyopangwa. Kama ni
mshambuliaji basi atazame zaidi kazi yake ya kufunga na si kuangalia kazi ya
mwenzake. Japokuwa mpira wa kisasa ni kushirikiana, lakini watatikiwa kutimiza majukumu
yao kwanza na baada ya hapo kuwasaidia wenzao. Sio beki muda wote anawaza
kwenda kushambulia wakati jukumu lake la kwanza ni kulinda lango lake. Aende
kushambulia kama kuna uwezekano na wapinzani hawawezi kuleta matatizo.
Tatu; wachezaji wa Taifa stars watatakiwa kucheza
kitimu na si kibinafsi. Asitokee mchezaji anayetaka kuonekana ni nyota zaidi ya
wengine. Wote watatakiwa kucheza kwa mtazamo wa kitimu na kusaidiana kwa kila
namna. Kama ni mshambuliaji asilazimishe kufunga wakati hawezi. Atoe pasi kwa
mwenye nafasi ili timu ipate matokeo. Hakuna faida ya kuonekana nyota wakati
timu haina matokeo mazuri.
Nne; wachezaji wa Stars wanatakiwa kuulinda mpira.
Wasiruhusu wapinzani kupora mipira kirahisi. Wakae na mpira, wacheze kwa kwenda
mbele na kutengeneza nafasi za kufunga.
Tano; wasikate tamaa. Wanatakiwa kupambana dakika
ya kwanza mpaka dakika ya mwisho. Hata kama watafungwa mapema, cha msingi ni
kuendeleza mapambano mpaka kipyenga cha mwisho. Kama watajaribu kukata tamaa
kwasababu wamefungwa au wameshindwa kupenya ngome ya Zimbabwe, basi malengo yao
hayatatimia.
Sita; watakiwa kujenga mashambulizi ya kasi ili
kuwavuruga Zimbabwe. Samatta na Ulimwengu watakiwa kwenda mbele kwa kasi, huku
viungo wa stars wakijaribu kupiga pasi za mwisho. Kama watacheza kwa staili hii
basi kuna uwezekano wa kufunga magoli mengi.
Saba; Taifa stars watakiwa kuimarisha zaidi safu
ya ulinzi. Wasije kuacha nafasi za wazi, kwasababu itaweza kuwaathiri. Erasto
Nyoni, Oscar Joshua, Nadir Haroub `Canavaro`, Agrey Moris na Kelvin Yondani
watatakiwa kujenga ngome imara ili kuwanyima Zimbabwe haki ya kufunga.
Nane; watatakiwa kuwasoma wapinzani wao jinsi
wanavyocheza na kuepuka kulazimishwa kucheza kama watakavyo Zimbabwe. Watatakiwa
kutumia muda kusoma mchezo wa vijana hawa wa Mugabe.
Tisa; nahodha Nadir Haroub `Canavaro` na kocha Mart
Nooij watatakiwa kuwahimiza wachezaji muda wote na kuwafanya wajitume dakika
zote. Itakuwa muhimu kukumbushana majukumu.
Kumi: wachezaji kamwe wasifikirie kuwa hawawezi. Lazima wajiamini hata kama Zimbabwe
wataonekana kuwa bora zaidi yao.
Haya si mambo pekee yatakayowapa Taifa stars
ushindi dhidi ya Zimbabwe hapo kesho. Yapo mengi lakini kwa leo haya yanatosha.
Kama una yako pia toa maoni yako ili kwa pamoja tujenge.
Mtandao huu unawatakia kila la heri Taifa stars
katika mechi ya kesho. Watanzania tuwe nyuma ya vijana wetu.
0 comments:
Post a Comment