Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MICHUANO mipya ya CECAFA Nile Basin Cup inatarajia
kuanza kutimua vumbi hapo kesho (juni 22) mwaka huu, lakini wawakilishi wa
Tanzania, Mbeya City fc mpaka muda huu wapo jijini Dar es salaam, huku hatima
yao ikiwa matatani.
Musa Mapunda, mwenyekiti wa Mbeya City fc
ameuambia mtandao huu kuwa mpaka usiku huu hawajapata tiketi za safari hiyo na
mbaya zaidi hakuna mawasiliano yoyote kutoka CECAFA wala TFF.
“Tupo Dar es salaam mpaka sasa. Michuano inaanza
kesho. Tungejua tusingeihamisha timu Mbeya. Tunatumia gharama zetu hapa Dar. Ni
hasara kubwa kwa klabu”. Alisema Mapunda.
Chama cha soka nchini Sudan kwa kushirikiana na
serikali ndio wadhamini wa mashindano hayo na wao ndio wanaobeba gharama zote.
Mbeya city fc wanatarajia kuanza kampeni zao juni
23 mwaka huu dhidi ya El Mereikh ya Sudan.
Hata hivyo walihitaji kuondoka juzi ili angalau
kupata siku mbili tatu kwa ajili ya kuzoea hali ya hewa ya Sudan ambayo ni joto
sana.
Wachezaji wa klabu hiyo wamezoea ubaridi wa Mbeya,
hivyo mazingira ya Sudan yatakuwa mapya
kwao na ndio maana walihitaji kwenda mapema.
Kwasasa kikosi cha Mbeya City kinaendelea na
mazoezi yake katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.
Kocha msaidizi wa klabu hiyo, Maka Mwalwiysi
amesema kwa asilimia kubwa kikosi kipo salama na wachezaji wapo katika morali
kubwa.
“Tumeshaiandaa timu vizuri na kinachosubiriwa ni
kukamilika kwa taratibu za safari. Ni michuano mizuri kwetu na tunaamini
tutafanya vizuri licha ya uchanga wetu”. Alisema Maka.

0 comments:
Post a Comment