Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976
MABINGWA watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara
wanatarajia kushuka dimbani jumapili ya wiki hii kuwakabili maafande wa JKT
Ruvu kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Kikosi cha Yanga chini ya kocha mkuu, Mhoalanzi
Hans Van der Pluijm kimeingia kambini jana jioni katika Hoteli ya Kiromo, huku kikiendelea kufanya mazoezi katika Uwanja
wa Boko Beach Veterani.
Yanga waliopo nafasi ya
pili kwa kujikusanyia pointi 46, pointi 7 nyuma ya Azam fc wenye pointi 53,
watakuwa wanacheza mechi ya raundi ya 23 jumapili, huku wakisubiri kiporo chao
dhidi ya Kagera Sugar aprili 9 mwaka huu uwanja wa Taifa, jijini Dar es salaam.
Mechi iliyopita jijini Tanga, Yanga
walipoteza mchezo kwa kipigo cha mabao
2-1 dhidi ya wenyeji wao, Mgambo JKT na kuweka rehani ubingwa wao msimu huu.
Yanga wamebakisha mechi nne na kama
watashinda zote watafikisha pointi 58
ambazo Azam fc pekee ndio wataweza kuzifikia kama watashinda mechi zao
tatu zilizosalia.
Hata hivyo taarifa njema kwa mashabiki
wa Yanga ni kuwa Mlinda mlango Deoragtias Munish "Dida" aliyekuwa
majeruhi kwa takribani wiki mbili, ameshapona majeraha na ameungana na wenzake kambini tayari kwa
maandalizi ya mchezo huo.
Mlinda Mlango wa Yanga, Juma Kaseja hajasimamishwa
Katika hatua nyingine, Yanga kupitia
tovuti yao rasmi wamekanusha taarifa zinazosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari
kwamba wachezaji wake, kiungo, Athuman Idd, beki Kelvin Yondani na Mlinda
mlango, Juma Kaseja wamesimamishwa kutokana na timu kufungwa na Mgambo JKT.
“Taarifa hizo hazina ukweli, wachezaji hao hawajafukuzwa na
wapo wanaendelea na mazoezi pamoja na wenzao”. Alifafanua taarifa ya Yanga.
Pia Yanga
wameviomba vyombo vya kutoa taarifa za
ukweli na sio kupotosha jamii na mwisho wa siku kuwapa usumbufu viongozi
kufanya kazi ya kukanusha.
Mchezo wa jumapili utakuwa mgumu kwa
timu zote kutokana na kusimama maeneo mawili tofauti kwenye msimamo wa ligi
kuu.
Yanga wapo nafasi ya pili na wanapambana
kutetea ubingwa wao walioutwaa msimu huu.
Wataingia katika mchezo huo wakiwa na
kumbukumbu ya kuwafunga JKT Ruvu mabao 4-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza
mwaka jana.
Haitakuwa kazi nyepesi kwa Yanga
kumfunga aliyekuwa kocha wake msaidizi ambaye kwasasa ni Kocha mkuu wa JKT
Ruvu, Fredy Felix Minziro.
Minziro na kikosi chake wapo nafasi ya 9
kwa kushuka dimbani mara 23 na kujikusanyia pointi 28 kibindoni.
Kiungo, Athumani Idd `Chuji` (wa pili kulia) hajasimamishwa
Maafande hao wataingia uwanjani wakiwa
na kumbukumbu ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 mechi iliyopita dhidi ya
Vibonde, Rhino Rangers kwenye uwanja wa Azam Complex.
Mechi ya jumapili ni muhimu kwao
kwasababu wanahitaji zaidi pointi ili kujiweka mazingira mazuri ya kubakia ligi
kuu.
Uzoefu unaonesha kuwa timu zilizopo
katika hatari ya kushuka daraja huwa zinacheza kwa kujituma zaidi, na ndio
maana Mgambo JKT walipambana na Yanga ndani ya dakika zote 90 na kushinda.
Kwa jicho la harakaharaka, unaweza
kuwapa asilimia kubwa Yanga kuwa watashinda mchezo huo, kutokana na mazingira
yao.
Kupoteza au kutoa sare kutazidi kuwaweka
Yanga mazingira magumu zaidi ya kutetea
ubingwa wao.
Matokeo yanayowafaa pekee ni ushindi,
kwasababu moto wa Azam fc kueleka kutwaa ubingwa ni mkali sana.
Itakuwa mechi muhimu kwa Yanga, na kocha
mkuu Pluijm atahitaji kutuliza akili zake kwani sasa matokeo hayatabiriki.
Haikuwa rahisi kuamini kama Mgambo
wangewafunga Yanga waliokamilika pale Mkwakwani, lakini mpira una matokeo ya
ajabu wakati fulani.
Yanga wanatakiwa kuingia jumapili kwa
tahadhari kubwa kwasababu kiwango cha sasa cha JKT Ruvu si cha kubeza. Wanaweza
kufanya lolote na kuwaharibia zaidi wanajangwani.

0 comments:
Post a Comment