..........................................
Na Baraka Mpenja wa fullshangwe, Dar es salaam
0712461976 au 0764302956
KINYANG`ANYIRO cha ubingwa wa
ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2013/2014, bado kinabaki kuwa kitendawili
kwa timu zilizopo juu katika msimamo.
Sare ya bao 1-1 jana uwanja
wa Taifa jijini Dar es salaam baina ya vinara Azam fc dhidi ya Yanga imezidi
kuweka mazingira magumu kwa mabingwa watetezi, Young African.
Katika mchezo huo uliovuta hisia za mashabiki, Yanga walikuwa wa
kwanza kufunga bao kipindi cha kwanza kupitia kwa Didier Kavumbagu, lakini Azam
fc walisawazisha dakika za lala salama kupitia kwa kinda, Kevin Friday.
Hiyo ilikuwa mechi ya 19 kwa
Yanga, wakati kwa Azam fc ilikuwa ya 20,
huku wakijikusanyia pointi 44, wakati Wanajangwani wakivuna pointi 40 katika
nafasi ya pili.
Yanga SC wamebakiza mechi 7,
wakati Azam fc wamebakiza mitanange 6.
Hamis Kiiza akitafuta njia ya kumkaba mchezaji wa Azam fc
Wikiendi hii timu zote
zitashuka dimbani. Yanga watasafiri mpaka mkoani Tabora kuwafuata maafande wa
Rhino Rangers, wakati jumapili machi 23, Azam fc watawakaribisha JKT Oljoro, uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Rhino Rangers ndio
wanaoburuza mkia katika msimamo wakiwa wameshacheza mechi 21 na kujikusanyia
pointi 13 tu kibindoni.
Kwa asilimia kubwa, maafande
hawa wa Tabora, wameshachungulia kushuka daraja na inawezekana hakuna muujiza
wa kubaki ligi kuu msimu huu kwasababu ya mazingira yao.
Mchezo dhidi ya Yanga utakuwa
mkali endapo bado Rhino wanahitaji ushindi.
Lakini imani yao imeshuka na
wanacheza bora liende na wameshapoteza matumanini ya kuendelea kucheza ligi
kuu.
Pointi 13 kwa mechi 21 ni
chache sana, zinahitajika nguvu za ziada kushinda mechi zote 5 walizobakiza,
hapo sasa tunaweza kuzungumza mengine.
Yanga wataingia uwanjani
wakiwa ma matokeo ya sare ya jana na suluhu ya Mtibwa Sugar wiki iliyopita
uwanja wa Jamhuri.
Yanga sc hawajafanya vizuri
mechi zao mbili tangu watolewe na Al Ahly ligi ya mabingwa kwa penati 4-3, machi
9 mwaka huu, jijini Alexndria, hivyo
hawana cha kuwaza zaidi ya ushindi.
Mtatwaa Ubingwa? : Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao la Didier Kavumbagu jana uwanja wa Taifa
Kama watashindwa kupata
ushindi katika mchezo huo, watakuwa wanazidi kuweka rehani ubingwa wao msimu
huu.
Kwa maana hiyo, kocha mkuu wa
Yanga, Hans Van Der Pluijm lazima awaeleze vijana wake umuhimu wa mechi ya jumamosi
endapo wanahitaji ketetea taji lao.
Wakati Yanga wakiwa kwenye
mawazo mazito juu ya mchezo huo, wapinzani wao, Azam fc watakuwa wanasubiria
matokeo ili kujipanga kwa mchezo wa kesho yake.
JKT Oljoro waliopoteza matumanini ya kusalia ligi kuu
msimu , wataingia kuwavaa Azam fc ambao hawajapoteza mchezo mpaka sasa kwa
lengo la kutafuta pointi tatu.
Mechi za karibuni zinaonesha
kuwa Azam fc wamekuwa bora zaidi katika uwanja wao kwasababu wanagawa dozi kubwa kwa wapinzani.
Mechi iliyopita waliwafunga
Coastal Union mabao 4-0, hivyo JKT Oljoro wasipokuwa makini watachezea kipigo.
Endapo Azam fc watashinda mechi
hiyo, watazidi kujikita zaidi kileleni, nao Yanga wakishinda watandelea kuwa wa
pili.
Matokeo ya sare au suluhu
hayatakuwa mazuri kwa Yanga, kwasababu Mbeya City waliopo nafasi ya tatu nao
watacheza na JKT Ruvu jumamosi uwanja wa Chamazi.
Kama Yanga hawatashinda na
Mbeya City wakapata matokeo ya ushindi, basi Yanga watashuka nafasi ya tatu.
Hata kama watatoa sare au
suluhu mjini Tabora, bado Yanga watabaki nafasi ya tatu, kwani Mbeya City watakuwa
wamefikisha pointi 42, Yanga 41.
Kama Yanga watashinda na
Mbeya City watashinda, basi nafasi za pili na tatu zitabaki kama zilivyo.
Matokeo yoyote ya Yanga na
Mbeya City hayatakuwa na athari kwa Azam fc katika nafasi ya kwanza, isipokuwa
watasogelewa kwa pointi.
Wakati Yanga na Azam fc
wakichunao vikali kusaka ubingwa, mechi zilizosalia kwa timu zote ni kama
zifuatazo;
Yanga wamebakiza mechi dhidi
ya Rhino Rangers itakayochezwa machi 22 mwaka huu uwanja wa Ali Hassan Mwinyi
mjini Tabora.
Baada ya hapo atakuwa na mechi
dhidi ya Tanzania Prisons uwanja wa Taifa.
Ugumu wa mechi hizi mbili unatokana
na mazingira ya Prisons na Rhino kwa sasa.
Hawataki kushuka daraja, zaidi
Prisons wamedhamiria kubakia lihi kuu kuliko Rhino wanaoonekana kukata tamaa.
Haitakuwa kazi nyepesi kwa
Yanga kuwafunga wajelajela hao uwanja wa Taifa, jijini Dar es salaam.
Mechi nyingine zilizosalia
kwa Yanga ni dhidi ya Mgambo JKT, Uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Hii pia itakuwa na changamoto
kubwa kwasababu Mgambo wanajinusuru kushuka daraja msimu huu.
Pia Yanga wamebakiza mechi dhidi ya Kager Sugar, Uwanja wa Taifa,
mechi dhidi ya JKT Oljoro, jijini Arusha, mechi na JKT Ruvu uwanja wa Taifa.
April 19 mwaka huu Yanga
watafunga msimu kwa kuvaana na Simba sc uwanja wa Taifa.
Katika mechi saba zilizosalia
kwa Yanga, mechi mbili pekee ndizo atakutana na timu zilizopo salama msimu huu
na zinahitaji nafasi nne za juu.
Kagera Sugar mpaka sasa wana
uhakika wa kusalia ligi kuu pamoja na Simba sc ambao wanasaka nafasi za juu.
Mechi nyingine zote, Yanga
atakutana na timu zinazopambana kukwepa mkasi wa kushuka daraja. Hivyo lazima
ajiandae kwa nguvu zote kwasababu kukamiana kutakuwepo.
Kila timu inahitaji kupata
ushindi bila kujali inakutana na timu kubwa au ndogo.
Kocha wa Yanga , Mholanzi,
Hans Van Der Pluijm akisaidiwa na Charles Mkwasa wanahitaji kutuliza sana akili zao kuelekea mechi hizo.
Azam fc amebakiza mechi sita
ambazo ni dhidi ya JKT Oljoro, Mgambo, Ruvu shooting, JKT Ruvu, Mbeya City na
Simba sc.
Mechi dhidi yaMbeya City
itakayopigwa sokoine Mbeya, itakuwa ngumu zaidi kwa Azam fc kulingana na rekodi
ya Mbeya City katika uwanja wake.
Mbeya City hawajawahi
kufungwa kwao, hivyo lazima Azam fc wajiandae kama wanataka kuvunja rekodi hii.
Pia Mbeya City wanasaka
ubingwa wa kwanza kama ilivyo kwa Azam fc. Tofauti ni umri katika ligi. Azam fc
waliingia 2008/2009, Mbeya City waliingia 2013/2014.
Azam fc ameshakuwa makamu
bingwa kwa zaidi ya misimu miwili, wakati Mbeya City ndio kwanza wanaanza
kutafuta mafanikio.
Mechi hii itakuwa ngumu kwa
timu zote mbili, matokeo yatategemea jinsi makocha wote wawili, Juma Mwambusi wa
Mbeya City na Mcameroon, Joseph Marius Omog wa Azam fc wamejipangaje.
Pia mechi dhidi ya Simba sc
itakuwa mlima mwingine kwa Azam fc kwasababu Simba hawatakuwa na chakupoteza
zaidi ya kusaka ushindi.
Kwa mazingira ya mechi za
Azam fc, itakuwa ngumu kwake kupata ushindi kwenye baadhi ya mechi kwasababu
wapinzani wake wanahitaji kujiweka vizuri katika msimamo.
Simba na Mbeya City wanawania
nafasi za juu. Ruvu Shhoting anatafuta nafasi nzuri pia.
Mgambo, JKT Ruvu, JKT Oljoro
wapo katika hatihati ya kukwepa kushuka daraja, hivyo mechi zao zitakuwa ngumu
zaidi kutokana na kukutana na timu ambayo inaongoza ligi.
Haitakuwa kazi nyepesi kwa
Azam fc kuibuka na ushindi katika mechi hizi, lakini kama watajiandaa vizuri
basi wataweza kuvuna ushindi na kujihakikishia kutwaa ubingwa msimu huu.
Ligi ya mwaka huu imekuwa na
changamoto kubwa kutokana na timu kubwa za Simba na Yaga kushindwa kufua dafu
kwa Azam fc na Mbeya City.
Misimu ya nyuma, mpaka sasa ilikuwa
rahisi kubashiri bingwa, na wakati mwingine timu ilikuwa inatangaza ubingwa
kabla ya mechi tatu au nne.
Kwa msimu huu jambo hilo
limebaki kuwa ndoto, ubingwa utaonekana mechi za mwisho, kwani mpaka sasa mbio
bado zipo wazi kwa klabu zaidi ya moja.
Katika soka, hii ni hatua
nzuri kwasababu inadhirisha zimekuweo timu zaidi ya mbili zenye ubora wa juu,
tofauti na miaka ya nyuma iliyokuwa na ufalme wa Simba na Yanga.
Tuzidi kusubiri ili kuona
nani ataibuka kidume katika nafasi nne za juu.
0 comments:
Post a Comment