Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976 au 0764302956
WANA Lambalamba Azam fc wamesema nia yao ya kutwaa
ubingwa kwa mara ya kwanza msimu huu iko palepale japokuwa kuna ushindani
mkubwa.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo wa kesho dhidi ya
Coastal Union katika uwanja wa Azam Complex , uliopo Chamazi, nje kidogo ya
jiji la Dar es salaam, afisa habari wa klabu hiyo, Jafar Idd Maganga amesema
kila kitu kinakwenda sawa.
“Msimu huu ligi imekuwa ngumu zaidi, kila timu
imejipanga na ndio maana matokeo yasiyotegemewa yanapatikana. Sisi tunaendelea
kupambana ili tubaki kileleni na kutwaa ubingwa wetu wa kwanza ligi kuu
Tanzania bara”. Alisema Jafar.
“Coastal ni timu nzuri yenye ushindani mkubwa.
Tunajua ugumu wa mchezo huo, lakini kocha wetu Joseph Marius Omog amewaandaa
vijana wetu kutafuta ushindi”. Alisema Jafar.
Aidha Afisa habari huyo aliongeza kuwa hakuna timu dhaifu
msimu huu na ndio maana timu inatoka kufungwa 6-0 halafu unakutana nayo
inakufunga.
“Sisi ni timu pekee ambao hatujapoteza mchezo mpaka
sasa. Malengo yetu ni kuktwaa ubingwa msimu huu. Tutapambana mpaka mwisho tuone
matokeo yake”. Alisisitiza Jafar.
Naye Afisa habari wa Coastal Union, Hafidh Kido
aliandika kwenye mtandao wa klabu hiyo kuwa wamejiandaa kukabiliana na kikosi
cha Azam fc.
“Azam ni wazuri na hawajafungwa. Sisi pia ni wazuri,
lakini hatujawa na matokeo mazuri sana. Tumejiandaa kupambana mwanzo mwisho
katika mechi yetu hiyo muhimu ili kupata pointi tatu muhimu”. Alisema Kido.
Mpaka sasa Azam fc wapo kileleni wakiwa na pointi 40,
wakati Coastal Union wao wapo nafasi ya
7 wakiwa na pointi 26.
Mechi nyingine itachezwa Uwanja wa Kaitaba mjini
Bukoba kwa kuwakutanisha wenyeji Kagera Sugar dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons
kutoka jijini Mbeya.
Nao Mabingwa watetezi Yanga wataumana na Mtibwa
Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
0 comments:
Post a Comment