Na Aron Msigwa – MAELEZO, Dar es salaam.
Serikali
imewataka wananchi kuzitumia ipasavyo fursa za elimu zinazotolewa
kupitia programu mbalimbali za ikiwemo Elimu ya Watu Wazima (EWW) na ile
ya Elimu Nje ya Mfumo Rasmi (ENMRA) ili kupunguza tatizo la umasikini,
maradhi na ujinga.
Kauli
hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Mkuu wa mkoa wa Dar es
salaam Bw. Said Meck Sadiki wakati akitoa taarifa kwa wananchi wa mkoa
wa Dar es salaam kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Elimu ya Watu Wazima na
Elimu Nje ya Mfumo Rasmi yatakayofanyika jijini Dar es salaam kuanzia
Novemba 13, 2013 yakiongozwa na kauli mbiu “Kisomo kwa ajili ya Karne ya
21”
Amesema
serikali imeanzisha programu mbalimbali za elimu kuanzia msingi mpaka
sekondari kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata fursa hiyo na
kuondokana na tatizo Umaskini, maradhi na ujinga na kuwawezesha
kujikwamua kiuchumi, Kijamii, Kisiasa na Kiutamaduni.
Ameeleza
kuwa mkoa wa Dar es salaam kwa sasa unaratibu program mbalimbali
zikiwemo Mpango wa Elimu ya Msingi kwa walioikosa (MEMKWA) unaowahusisha
wanafunzi wenye umri kati ya miaka 9 hadi 18 ambao husoma katika mfumo
wa makundi rika.
Amesema
jumla ya wanafunzi 1,846 wamejiunga na program hiyo kwa mwaka 2013
wakihusiha wale wenye umri wa miaka 9 mpaka 13 na 14 mpaka 18.
Bw.
Meck Sadiki ameeleza kuwa mkoa wa Dar es salaam pia unasimamia Mpango
wa Uwiano kati ya Elimu ya Watu Wazima na Jamii (MUKEJA) unaohusu utoaji
wa Elimu kupitia kisomo cha kujiendeleza na kisomo chenye manufaa
kinachowahusisha watu wazima wenye umri zaidi ya miaka 18 wapatao 1,678
waliojiunga kwa mwaka 2013.
Ameongeza
kuwa wanafunzi wapatao 2,309 wamejiunga na programu ya Elimu ya
Sekondari Huria (PESH) ambayo huendeshwa kwa wanafunzi ambao wamekosa
sifa za kuchaguliwa kujiunga na shule za sekondari kupitia chaguo la
mfumo rasmi.
“Wanafunzi
wanaosoma katika mpango wa PESH serikali imewawekea utaratibu wa kusoma
katika shule za msingi na sekondari ambazo hazina utaratibu wa awamu
mbili za kusoma, wao husoma jioni baada ya muda wa kawaida wa masomo”
Aidha
amezitaja programu nyingine za elimu zinazowahusisha watu wazima na
vijana kuwa ni pamoja na Elimu ya Masafa na Ana kwa Ana (ODL) ambayo ina
jumla ya wanafunzi 335 wanaoendelea na masomo na Elimu Changamani
(IPPE) ambayo inawahusisha vijana 112 waliomaliza elimu ya msingi na
kukosa nafasi ya kujiunga na sekondari ambao hujengewa uwezo katika
masomo ya maarifa, ufundi, afya, maktaba na mazingira.
Kuhusu
maadhimisho ya mwaka huu Bw. Mecki Sadiki ameeleza kuwa pamoja na
mambo mengine yatakuwa na mchango mkubwa katika kuhamasisha jamii
kushiriki kikamilifu kusikiliza, kusoma na kutoa maoni ya upatikanaji wa
katiba mpya nchini, kuongeza mwamko kwa jamii katika masuala ya elimu,
kutathmini utekelezaji wa azimio la ulimwengu kuhusu utoaji wa elimu kwa
wote na kutathmini mafanikio na mapungufu ya utekelezaji wa Elimu ya
Watu Wazima (EWW) na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi (ENMRA).


0 comments:
Post a Comment